Kumbukumbu ya miaka 30 ya Chernobyl | Masuala ya Jamii | DW | 26.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Kumbukumbu ya miaka 30 ya Chernobyl

Ukraine leo inaomboleza ajali mbaya zaidi ya kinyuklia ya Chernobyl iliotokea miaka 30 iliyopita. Maombolezo hayo yameongozwa na rais Petro Poroshenko. Jamaa na familia walifanya maombi na kuwasha mishumaa.

Eneo la mkasa wa Charnobyl nchini Ukraine

Eneo la mkasa wa Charnobyl nchini Ukraine

Ukraine leo inaomboleza ajali mbaya zaidi ya kinyuklia ya Chernobyl iliotokea miaka 30 iliyopita. Maombolezo hayo yameongozwa na rais Petro Poroshenko na mkuu wa Benki ya Ulaya ya ujenzi na maendeleo ambayo inasimamia hifadhi ya eneo hilo Suma Chakrabarti.

Jamaa na familia za waliofariki walifanya maombi na kuwasha mishumaa katika kanisa lililoko mjini Kiev lililojengwa kama ukumbusho. Maombi mengine pia yamefanywa katika mji wa Slavutych ulioko kilomita 50 kutoka Chernobyl.

Mkasa huo uliacha sumu ya kudumu katika maeneo mengi Ulisababisha mataifa ya marekani na Ulaya kupunguza sana matumizi ya nguvu ya nyuklia katika viwanda vyao. Kadhalika ajali hiyo ilichangia kuibuka kwa vyama vya kutetea mazingira nchini Ujerumani maarufu kama Green Parties na mataifa mengine ya Ulaya ambayo awali yalitegemea pakubwa nishati ya nyuklia.

Uwanja wa michezo ulioharibiwa na mkasa wa Charnobyl.

Uwanja wa michezo ulioharibiwa na mkasa wa Charnobyl.

Maafa ya Chernobyl katika wakati huo Ukraine ilipokuwa Jamhuri moja wapo ya zile zilizounda muungano wa Kisovieti au Urusi ya zamani, yalisababishwa na jaribio la usalama lilokwenda kombo kwenye mtambo wa nne wa nyuklia na kusasabisha mawingu ya vitu vya nyuklia kutanda barani kote Ulaya.

Juhudi za serikali

Maafa hayo na jinsi serikali ilivyoyashughulikia ikiwa ni pamoja na amri ya kuondolewa kwa wakaazi kutolewa tu baada ya masaa 36 ya kutokea kwa ajali hiyo imeonyesha mapungufu ya mfumo wa utawala wa Kisovieti na urasimu wake usiohesabika pamoja na utamaduni wa siri uliojengeka.

Mikhail Gorbachov alisema analiona janga hilo la Chernobyl kuwa mmojawapo wa misumari ya mwisho kwa Muungano wa Kisovieti ambao hatimaye ulisambaratika hapo mwaka 1991.

Ajali hiyo iliuuwa watu 31 papo hapo na kuwalazimisha maelfu wengine kukimbia makaazi yao. Idadi kamili ya vifo kutokana na sumu ilosababishwa na sumu ya mionzi ya nyuklia kwa kusababisha maradhi kama vile satarani bado iko kwenye mjadala.

Repoti ya shirika la kimataifa la mazingira la Greenpeace iliyotolewa kabla ya kumbukumbu hii imetaja utafiti uliofanywa na Belarus ulikadiria jumla ya vifo vya satarani kutokana na ajali hiyo kufikia 115,000 kinyume kabisa na makadirio ya shirika la Afya Duniani WHO ya vifo 9,000.

Rais wa Ukraine Petro Poroschenko akiweka shada la maua kwenye kituo cha kumbukumbu mjini Kiev.

Rais wa Ukraine Petro Poroschenko akiweka shada la maua kwenye kituo cha kumbukumbu mjini Kiev.

Utafiti huo wa Greenpeace pia umebaini kwamba watu wanaoishi katika eneo hilo la ajali bado wanaendelea kunywa na kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha sumu ya nyuklia.

Utafiti huo umesema hususan kanda iliokuwa imetengwa karibu na uliokuwa mtambo wa nyuklia wa Chernobyl linaendelea kuathiriwa na viwango vya juu ya sumu na halifai kuishi watu.

Walionusurika wangali wanakumbuka

Lakini halimshughulishi sana Lozbin mmojawapo ya watu 160 wanaokadiriwa kurudi tena katika kanda hiyo anasema hakuna cha kuogopa.

Amesema hataki kwenda mji mkuu wa Kiev na kuacha mazingira hayo mazuri ya asili ambapo unaweza kusikia sauti za ndege na kuku.

Maria Lozbin anafuga kuku na bata na anaotesha mbatata na nyanya na pia huchuma uyoga ulioko kwenye msitu wa karibu.

Anasema mahala hapo hakuna miale ya sumu ya nyuklia na haogopi kitu na itakapofika wakati wa kufa hatokufa kutokana miale ya sumu ya nyuklia.

Maria mwenye umri wa miaka 69 alikuwa miongoni mwa maelfu kwa maelfu ya watu kuhamisha kutoka kwenye nyumba zao baada ya kutokea kwa ajali hiyo ya nyuklia ya Chernobyl hapo mwezi wa Aprili mwaka 1986 lakini amerudi tena na familia yake ya watu sita miaka sita iliopita kuishi kwenye ardhi ndani ya kanda iliotengwa ya kilomita 30 ambapo hatari ya sumu za miale ya nyuklia inatajwa kubwa bado ingalipo.

Mwenyekiti wa chama cha kumbukumbu ya wahanga wa Chernobyl Nail Mardagalimov.

Mwenyekiti wa chama cha kumbukumbu ya wahanga wa Chernobyl Nail Mardagalimov.

Kwa wale wanaorudi katika mji walikozaliwa wa Priyat kwa kumbukumbu hiyo hisia walizonazo ni mchangayiko wa kumbukumbu za kuchangayikiwa na kujitowa muhanga.

Mahala kulikokuweko nyumba yao sasa ni msitu Zoya Perevozechenko mwenye umri wa miaka 66 anakumbuka siku ya ajali hiyo kulikuwa na joto kali na watu walikuwa wamevaa vifuniko vya uso hawakuelezewa kitu mambo yote yalikuwa siri.

Mumuwe aliyekuwa akifanya kazi kama msimamiz katika kulikotokea ajali alikuwa ni miongoni mwa watu 31 waliokufa kutokana na miale ya sumu ya nyuklia iliosababaishwa na ajali hiyo.Alipelekwa Mosco kwa mataibabu lakin alikufa siku 45 baadae yeye na watoto wake wadogo wa kike waliishi Kiev ambapo wanaishi hadi leo hii.

Wakati huo hakuna mtu aliyejuwa kwamba kuvuja kwa mtambo huo wa nyuklia katika lililokuwa jimbo la Muungano wa Kisoviet kulikuwa kukimwaga sumu angani yenye mionzi mikali ya nyuklia ambako kutakuja kuwa ajali mbaya kabisa ya nyuklia duniani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/John Juma/Reuters/AP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com