Kumbe Barrow alimkubalia Jammeh aondoke na utajiri ′wake′ | Matukio ya Afrika | DW | 25.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

GAMBIA

Kumbe Barrow alimkubalia Jammeh aondoke na utajiri 'wake'

 Imefahamika kuwa Rais Adama Barrow wa Gambia alifikia makubaliano na mtangulizi wake, Yahya Jammeh, yanayomruhusu Jammeh kubakia na magari yake ya kifahari ili naye akubali kwenda kuishi uhamishoni Guinea ya Ikweta.

Chanzo kimoja kwenye uwanja wa ndege wa Banjul kililiambia shirika la habari la AFP kwamba shehena ya magari ilikuwa ikipakiwa kwenye ndege usiku wa Jumamosi, siku ambayo Jammeh aliondoka nchini Gambia. 

"Rolls Royce mbili na Mercedes Benz moja ziliingizwa kwenye ndege ya mizigo ya Chad huku magari mengine 10 ya kifahari yakingojea kusafirishwa."

"Serikali ilikuwa imejitayarisha vya kutosha kutoa msaada mkubwa kwa Jammeh aondoke na matokeo yake ikaonekana ni bora aondoke na mali zake zote," alisema msemaji wa Barrow, Halifa Sallah.

Chanzo kilichoko uwanja wa ndege kinasema kuliwahi kuzuka mabishano baina ya serikali na upande wa Jammeh juu ya gari gani ipakiwe kwenye ndege baina ya Bentleys na Rolls Royce, kabla ya baadaye kukubaliana juu ya Rolls Royce. 

Habari hii huenda ikawakasirisha zaidi Wagambia ambao ndio kwanza wamejuwa kuwa Jammeh aliachiwa kuondoka na dola milioni 11 za serikali na kuiwacha hazina ya nchi ikiwa nyeupe.

"Nimefadhaishwa sana na makubaliano haya; lakini nakisia kuwa maisha ya mtu mmoja kutoka upande wowote ule yana thamani zaidi kuliko utajiri wote wa Jammeh," aliandika mtumiaji wa Twitter ajiitaye @YesWeCan_Gambia.

Wakati bei ya Rolls Royce moja ni dola 250,000, raia wengi wa Gambia wanaishi kwa chini ya dola 2 tu kwa siku.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com