1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Kuleta amani kwa kutumia silaha - halitawezekana"

Maja Dreyer11 Januari 2007

Mkakati mpya wa rais Bush leo hii umepiga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani ya leo hii, pamoja na sera mpya za nishati za Umoja wa Ulaya zilizotangazwa jana.

https://p.dw.com/p/CHTz

Tukianza na gazeti la “Thüringische Landeszeitung” la mjini Weimar tunasoma ukosoaji mkali wa sera mpya aliyoitangaza Rais Bush wa Marekani. Gazeti hilo limeandika:
“Kuumaliza mzozo huu wa Iraq kwa njia ya kijeshi haiwezekani, ikiwa idadi ya wanajeshi itaongezwa kwa 20.000 au 50.000. Mkakati huo haukusaidia huko Vietnam, wala hautasaida katika vita vya Iraq. Hakuna pendekezo lolote la kutatua mivutano kati ya Wasunni na Washii, wala hakuna wazo vipi kuzihusisha nchi jirani katika kutafuta suluhisho.”

Tunaendelea la gazeti la “Bayerische Rundschau” ambalo limeandika yafuatayo:

“Kwa kupeleka wanajeshi wengi zaidi Iraq, George Bush, kwa mara nyingine tena, hakujali mapendekezo ya watoaji ushauri wa mambo ya usalama na ya wakuu wa majeshi. Wademokrats tayari waliarifu kuwa wanaupinga mpango wa Bush. Lakini tusisahau kuwa, hata wapinzani wa Bush hawajatoa pendekezo lao la kuiboresha hali ya usalama nchini Iraq.”

Na hatimaye kuhusu suala hilo hilo, sasa ni gazeti la “Nordbayerischer Kurier”. Mhariri wake aliandika:
“Kuleta amani kwa kutumia silaha – jambo hilo halitafanikiwa. Iraq inahitaji zaidi ya mkakati wa kijeshi tu. Sababu ya kuongezeka kwa idadi ya Wairaqi wanaoyaunga mkono makundi ya siasa kali sana ni kwamba watu hawa hawana matumaini tena maisha yao kuwa yatakuwa bora.”

Suala lingine linalozungumziwa na wahariri wa magazeti ya humu nchini leo hii ni sera mpya za nishati za Umoja wa Ulaya. Malengo ya sera hizo hasa ni kupunguza kuzitegemea nchi za nje katika kupata nishati pamoja na kupunguza utoaji wa gesi chafu. Haya basi ni maoni ya mhariri wa gazeti la “Mittelbayerische Zeitung”:
“Lengo zuri la kupunguza utoaji wa gesi chafu lazima lilinganishwe na hali halisi. Ni kwali kwamba duniani kote ni nchi za Ulaya ambazo zimefanikiwa zaidi katika kuihifadhi hali ya hewa. Lakini ni wazi kwamba hata nchi hizo zitashindwa kufikia malengo yaliyowekwa katika makubaliano ya Kyoto. Basi kinachotakiwa sasa ni hatua halisi badala ya maneno tu.”

Na mwishowe ni gazeti la “Märkische Allgemeine” la mjini Potsdam. Limeandika:
“Ili kushindana na China, Marekani na Urusi, Ulaya iwe na msimamo wa pamoja. Lakini hilo ndilo tatizo lake. Nchi za Ulaya haziwezi kukubaliana katika suala la nishati ya kinyuklia wala hazina sera ya pamoja kuhusu suala la nishati ya kutokea Urusi. Kwa hivyo, sera hizo mpya za nishati zitabakia kuandikwa kwenye makaratasi tu.”