Kujongeleana Korea mbili na China kama dola kuu magazetini | Magazetini | DW | 10.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Kujongeleana Korea mbili na China kama dola kuu magazetini

Mazungumzo kati ya wawakilishi wa Korea Mbili, uwezekano wa China kugeuka kuwa dola lenye nguvu zaidi ulimwenguni na mazungumzo ya kupima uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikuu magazetini

Tunaanzia katika rasi ya Korea ambako matumaini yamechomoza, pengine mfarakano kati ya ndugu hao wawili utamalizika baada ya pande hizo mbili kukubali kuketi katika meza ya mazungumzo. Gazeti la "Freie Press" linaandika:"Mazungumzo hayo ni ya maana kwa pande zote mbili: Yanaimarisha dhima ya Korea Kusini mbele ya Marekani. Seoul inajibebesha jukumu la yanayotokea katika rasi ya Korea. Kwa muda mrefu, risala za mtandaoni za rais wa Marekani Donald Trump zilimlazimisha kiongozi wa Korea ya Kusini asubiri ili kutoutia mashakani uhusiano pamoja na mshirika wao muhimu. Ikiwa mazungumzo hayatovunjika, basi rais Moon Jae In anaweza pengine hata kufikia makubaliano ya kurahisisha familia kuungana upya na mengi mengineyo ya maana kama hayo. Kwa upande wake, Kim Jong Un anaweza kutegemea kuona vikwazo dhidi ya nchi yake vikipunguzwa makali. Zaidi ya hayo anataka kusababisha mfarakano kati ya Seoul na Marekani. Na hilo hata wakorea ya kusini wanalijua."

China inahitaji nini kutambulikana kama dola lenye nguvu zaidi duniani?

Mada yetu ya pili magazetini inamulika uwezekano wa Jamhuri ya umma wa China kugeuka kuwa dola lenye nguvu zaidi ulimwenguni. Gazeti la "Rheinpfalz" linahisi nguvu za kiuchumi pekee hazitoshi. Gazeti hilo linaendelea kuandika: "Kama kiuchumi China inasonga mbele kwa ustadi mkubwa, lakini ili kutambulika kama dola linaloongoza ulimwenguni, panahitajika mengi zaidi ya nguvu za kiuchumi. China si dola kuu hivyo. Haina mfumo unaoifungamanisha na sehemu nyengine ya dunia. Hakuna filamu za China zinazoangaliwa kila mahala. Hakuna muziki kutoka China unaosikika katika kila pembe ya dunia. Kwa wakati wote ambao wachina watayakataa yote hayo, wataendelea kushindwa nguvu na sio tu ya Marekani bali pia na nchi za Ulaya."

Hatima ya mazungumzo ya kuunda seriklali ya muungano wa vyama vikuu GroKo

Mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano kati ya vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU/CSU na kile cha SPD yameingia katika siku yake ya nne hii leo. Gazeti la "Rhein Zeitung" linamulika hali namna ilivyo na kuandika: "Serikali ya muungano wa vyama vikuu, mashuhuri kwa jina GroKo, pindi ikiundwa, basi watu wasitegemee kutokea mabadiliko yoyote. Mambo yatakuwa kama yalivyokuwa. Na pia upande wa viongozi, Angela Merkel anaendelea kubebeshwa jukumu la kushindwa CDU katika uchaguzi mkuu uliopita . Miaka miwili kutoka sasa karata zitachanganywa upya kumchagua atakaeshika nafasi yake. Na Martin Schulz nae pia anaangaliwa kuwa mwenyekiti wa muda tu wa chama cha Social Democratic. Pindi mazungumzo ya kuunda serikali ya muunganmo wa vyama vikuu-GroKo yakishindwa kuleta tija na uchaguzi mpya kuitishwa, atakaekiongoza chama hicho cha SPD hatokuwa tena Martin Schulz.

 

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com