1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujitanua kwa IS Libya kwaongeza mahitaji ya silaha

Mtono, Lilian11 Machi 2016

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameliarifu Baraza la usalama la umoja huo kuwa kujitanua kwa kundi la IS nchini Libya, kunazifanya pande zinazogombana kutafuta silaha zaidi ili kukabiliana na kitisho cha kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1IBqJ
Tunesien Libyen Anti-Dschihadisten-Zaun
Picha: picture-alliance/dpa/M. Messara

Halikadhalika wataalamu hao wamesema IS imewaandikisha jeshini vijana wa makabila pamoja na makamanda wa zamani katika jeshi la aliyekuwa kiongozi wa Libya, Moammar Gaddafi.

Sehemu ya ripoti ya wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa, iliyo chini ya kamati ya vikwazo ya umoja huo, imesema wapiganaji hao wa jihadi, wameweka makao ya kudumu kwenye mji wanaoushikilia ulioko Pwani wa Sirte, na kuwaua wapinzani, na sasa kundi hilo limebaki kuwa sehemu muhimu kisiasa na kijeshi kwenye eneo hilo.

Kundi hilo la itikadi kali za kiislamu, limekuwa likizunguka kwenye barabara za Tripoli na Magharibi mwa mji wa Sabrata, likijinasibu uwepo wake, kupitia wapiganaji wake ambao ni raia na kigeni wanaotokea Uturuki na Tunisia. Wapiganaji wa itikadi kali, kutoka Kusini mwa jangwa la Sahara, hupitia Sudan ili kujiunga na kundi hilo, lililojikita kwenye mji wa Sirte na Benghazi, hali inayoongeza wasiwasi kwamba linaweza kutoa mafunzo kwenye maeneo mengi zaidi ya Afrika

Libya ilitumbukia katika machafuko tangu mwaka 2011.

Muammar Al Gaddafi Portrait
Kiongozi wa Zamani wa Libya Muammar al-GaddafiPicha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Libya ilitumbukia katika machafuko baada ya Umoja wa Kujihami, NATO, kuunga mkono vuguvugu dhidi ya utawala wa muda mrefu wa kidikteta wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Moamer Khadhafi mwaka 2011. Tangu wakati huo Libya imekuwa chini ya vikwazo vya silaha, ingawa ripoti hiyo inabainisha kuwa serikali inayotambuliwa kimataifa yenye makao yake mjini Tobruk, hivi karibuni ilipata ndege za kivita aina ya Mig-21F.

Ndege hizo zinaonekana kufanana na zile zinazomilikiwa na Misri, ingawa nchi hiyo imeiambia kamati ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa taarifa za kupelekwa ndege zake nchini Libya hazikuwa sahihi. Kamati hiyo inaendelea kuchunguza iwapo Uturuki, Umoja wa nchi za Kiarabu, na Sudan zimevunja makubaliano ya vikwazo vya silaha.

Kuibuka kwa Dola la Kiislamu nchini Libya, kunaweza kuongeza juhudi za kikanda na za kimataifa kuingilia kati, hali inayoweza kuchochea mvutano zaidi ikiwa haitashughulikiwa ipasavyo. Ingawa kundi hilo halina mamlaka kwenye mapato yatokanayo na mafuta, lakini uvamizi kwenye vyanzo vya mafuta unaweza kuwa ni kitisho kwenye hali ya uchumi wa Libya..

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: Gakuba Daniel.