1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Hezbollah kwazusha hisia tofauti

Nijimbere, Gregoire16 Julai 2008

Kundi la Hezbollah la Lebanon limesherehekea kuachiliwa huru wafungwa wake watano waliokuwa wakizuwiliwa nchini Israel akiwemo mfungwa wa muda mrefu Samir Kuntar. Lakini nchini Israel ni huzuni.

https://p.dw.com/p/EdhZ
Miili ya wanajeshi hao wa Israel Ehud Goldwasser na Eldad Regev imerejeshwaPicha: AP

Operesheni hiyo ya kubadilishana wafungwa imefanyika katika kituo cha Nakoura kwenye mpaka kati ya Israel na Lebanon ikisimamiwa na mafisa wa Msalaba Mwekundu. Kundi la Hezbollah limekabidhi miili ya wanajeshi wawili Ehud Goldwasser na Eldad Regev.

Israel kwa upande wake imewaachilia huru wafungwa watano wa Hezbollah akiwemo mfungwa wa muda mrefu kuliko wote Samir Kuntar ambae alikuwa gerezani nchini Israel tangu mwaka 1979 kwa hatia ya mauaji ya watu watatu wakati wa shambulio nchini Israel mwaka huo. Chama cha Hezbollah kimesherehekea operesheni hiyo ambayo kinaitafsiri kama ushindi. ´´Israel imerejesha mpiganaji wetu mashuhuri Samir Kuntar kwa Msalaba Mwekundu´´, amesema msemaji wa Hezbollah Wafik Safa. Samir Kuntar anatarajiwa kupokewa kama shuja nyumbani kwake.


Wakati kuna sherehe nchini Lebanon na katika eneo la Wapalestina la Ukanda wa Gaza linaloongozwa na chama cha Hamas, upande wa Israel ni huzuni kwa sababu ilikuwa hatua ngumu kwa Israel kumuachilia mfungwa kama Samir Kuntar, amesema msemaji wa waziri mkuu wa Israel Mark Regev.

Katika familia za marehemu wanajeshi hao wawili wa Israel ambao kukamatwa kwao kusini mwa Lebanon kulizusha vita vya zaidi ya mwezi 1 kati ya Israel na Hezbollah mwaka 2006, watu wamekusanyika baadhi yao wakishindwa kujizuwia.

Rais wa Palestina Mahmud Abbas amekaribisha hatua hiyo ya kubadilishana wafungwa ambayo imefikiwa kati ya Israel na Hezbollah . Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ambae yupo ziarani hapa Ujerumani, amezipongeza pande hizo mbili yaani Israel na Hezbollah kufanikisha shughuli hiyo. Ujerumani imesema hiyo ni hatua nzuri kisiasa na kibinaadamu. Naibu msemaji wa serikali ya Ujerumani Thomas Steg amethibitisha mjini Berlin, kwamba shirika la upelelezi la Ujerumani,BND, ndilo lilihusika na upatanishi katika makubaliano hayo ya kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Hezbollah.