1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kosovo yaadhimisha mwaka mmoja tangu ijitangazie Uhuru

17 Februari 2009
https://p.dw.com/p/GvYS
Bendera ni sehemu ya mapambo ya kuadhimisha mwaka wa Uhuru.Picha: DW

Leo tarehe 17 Februari. Kosovo inasherehekea mwaka mmoja tangu ilipojitangazia uhuru. Nyingi miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya kujihami ya NATO zimeitambua kuwa dola huru. Licha ya malalamiko ya Waserbia juu ya hatua hiyo yaliowasiloishwa katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa, nchi za magharibi zinataka kuisaidia Kosovo kuwa na utawala wa kisheria.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema kujitenga kwa Kosvo na Jamhuri ya Serbia kulikua ni " mafanikio ya Ulaya", huku mwenzake wa Uhispania miguel Angel Moratinos akiiona hataua hiyo kuwa ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa.

Kosovo ilitangaza uhuru wake mwaka mmoja uliopita tarehe 17 februari na kusababisha mgawanyiko ndani ya Umoja wa ulaya wenye wanachama 27, wakati nchi 22 ziliitambua kama doala mpya .

Halikadhalika hatari na athari za kujitenga kwa Kosovo zimezungumzwa kote duniani, kwa sehemu sababu ikiwa ni kwamba Kosovo ambayo ni yenye ukubwa takriban wa theluthi moja ya ardhi ya Ubeligiji na akiwa na wakaazi wengi wenye asili ya kialbania, itaendelea kutegemea msaada wa nchi tajiri kwa ajili ya mustakbali wake.

Mpango wa makadirio ya mahitaji yake ya fedha katika mkutano uliofanyika Brussels Julai mwaka jana, ulipata ahadi ya msaada wa wafadhili 65, wa euro bilioni moja na milioni 5, ukiwa kama msaada wa maendeleo kwa Kosovo. kati ya hizo euro milioni 550 zitatoka katika bajeti ya umoja wa ulaya na nyengine 300 milioni kutoka nchi mbali mbali wanachama kwa jumla.

Umoja wa Ulaya pia ulitaka kuimarisha kile kinachotiliwa mkazo, ambacho ni utawala wa kisheria katika Kosovo. Lakini ilichukua muda wa hadi Disemba mwaka jana kwa umoja huo kuweza kufungua ofisi ya ujumbe wake wa kusimamia kazi hiyo unaojulikana kama EULEX kwa ufupi.

Kuchelewa kwake kulitokana na sababu za kisiasa kuliko kuwa za kifedha, kwani shughuli zilizogharimu euro milioni 205 kuhusiana na kuitumwa polisi 1,900, majaji, waendesha mashitaka na maafisa wa forodha katika taifa hilo jipya la Balkan zilikamilika tangu mapema. Kamanda mkuu wa majeshi yanayoongozwa na NATO huko Kosovo, Meja Jenerali Emilio Gay anasema,"Mwanzoni mwa mwezi Februari tumeanza kutaoa mafunzo.Kipaumbele ni kuondoa mabomu yaliobaki ardhini, kupambana na moto yaani hatua za kuwalinda raia na sio kupambana nao. Jeshi la Kosovo lipewe mafunzo kufikia kipimo cha majeshi ya NATO."

Umoja wa Ulaya umekua ukitafuta utaratibu kwa miezi kadhaa, utakaosaidia ujumbe wake juu ya utawala wa kisheria kuratibu shughuli zake pamoja na ule wa Umoja wa mataifa UNMIK. ambao umeitawala Kosovo kwa miaka 9 iliopita.

Nchi za magharibi na Kosovo zilitaka EULEX ichukua nafasi ya ujumbe wa Umoja wa mataifa, lakini mpango huo ukashindwa baada ya Urusi kuzuwia kuondoka kwa ujumbe wa umoja wa mataifa katika Kosovo, ikitishia kutumia kura ya turufu.

Suala la utawala wa kisheria linazingatiwa kama kipa umbele kuishawishi Kosovo, kwamba inaweza hatimae ikaisaidia kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Lakini ujumbe huo wa EULEX unakabiliana na matatizo. Victor Reuter ni msemaji wa ujumbe huo wa umoja wa ulaya kuhusu utawala wa kisheria katika Kosovo akizungumzia hali hiyo anasema kuwa " Ni dahahiri kuwa matatizo yanakutikana kule kwenye uhalifu wa mpangilio na rushwa. Sisi tupo tayari kutekeleza jukumu letu .Wenyeji watakaposhindwa basi polisi, majaji na wanasheria wa EULEX wataingilia kati.

Kwa upande mwengine Serbia inaweza kutarajia kujiunga na mapema na umoja wa ulaya, ikiwa tu itasaidia kulitatua suala la washukiwa wa uhalifu wa kivita na pindi itaacha dai lake kwamba Kosovo ni sehemu ya ardhi yake.

wachambuzi wa mambo wanakubaliana kwamba umoja wa ulaya unajaribu kuzishawishi Kosovo na Serbia kwa masharti yake zikiwa na matumaini ya kujiunga na umoja huzuo, lakini kutokana na utata uliopo nafasi hiyo kwa saasa inaelekea iko mbali mno.Mustakbali wowote kuhusiana na Kosovo unaweza tu kufanikiwa kwa Urusi inayoonekana kuwa mshirika wa Serbia katika suala hilo kuondoa pingamizi.

Prema Martin /ZR/RTR