1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yatuhumiwa kuanza upya harakati za Nyuklia

Saumu Mwasimba
7 Machi 2019

Jeshi la Korea Kusini lasema linafuatilia kwa karibu vituo vya shughuli za Nyuklia vya Korea Kaskazini baada ya idara yake ya ujasusi kuwaambia wabunge kuna harakati mpya zilizogunduliwa kuendelea huko Korea Kaskazini

https://p.dw.com/p/3Eadx
Nordkorea Raketentest auf Startanlage Sohae
Picha: picture-alliance/Yonhap

Rais wa Marekani Donald Trump amesema atavunjwa moyo sana na kiongozi wa Korea Kaskazini  endapo ripoti zitathibitika kwamba Korea Kaskazini inakijenga tena kituo chake cha shughuli za Nyuklia. Taarifa kwamba nchi hiyo imeanza upya harakati hizo za silaha za Nyuklia zilitolewa na mashirika ya wataalamu ya Marekani na Korea Kusini.

Taasisi mbili za kitaalamu za Marekani na shirika la habari la Korea Kusini Yonhap waliripoti siku ya jumanne kwamba shughuli inaendelea ya kujenga tena sehemu ya kituo cha kurushia setalaiti cha Korea Kaskazini kwenye eneo la Sohae hata baada ya rais Trump kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un katika mkutano wa kilele mjini Hanoi nchini Vietnam wiki iliyopita. Ni taarifa hizi ndizo zinazompa wasiwasi rais wa Marekani ambaye amewaambia waandishi wa habari huko ikulu kwamba atavunjika sana moyo ikiwa taarifa hizo zitathibitika kuwa kweli.

USA-Nordkorea Gipfel - Donald Trump, Kim Jong Un
Picha: picture-alliance

Korea Kaskazini ilianza  harakati za kuharibu mtambo wake wa kuendesha majaribio ya makombora katika eneo la Sohae mwaka jana baada ya kutoa ahadi ya kuchukua hatua hiyo katika mkutano wa kwanza wa kilele uliofanyika baina ya kiongozi wake Kim Jong Un na Donald Trump mwezi Juni. Mkutano wa pili katika ya viongozi hao ulivunjika wiki iliyopita mjini Hanoi kufuatia tafauti zilizoibuka kuhusu suala la kwa umbali gani Korea Kaskazini iko tayari kupunguza mpango wa Nyuklia na nia iliyopo upande wa Marekani katika kulegeza vikwazo vyake dhidi ya Korea Kaskazini.

Vietnam l Hanoi, US-Präsident Donald Trump trifft den nordkoreanischen Staatschef Kim Jong Un
Picha: Reuters/L. Millis

Picha za Satelaiti zilizoonekana na wachunguzi wa 38 Noth ambao ni mradi wa Marekani kuhusu Korea Kaskazini zimeonesha kuna majengo katika eneo la kituo cha Nyuklia cha Sohae ambayo yalijengwa upya katika kipindi cha kati ya Februari 16 na Machi 2. Jeshi la Korea Kusini kwa upande mwingine limesema linafuatilia kwa makini harakati za Nyuklia za Korea Kaskazini na vituo vyake vya makombora baada ya idara ya ujasusi ya nchi hiyo kuwaambia wabunge kwamba harakati nyingine mpya zimegundulika katika kituo cha utafiti  ambako inasadikika nchi hiyo ya Korea Kaskazini inajenga makombora ya masafa marefu yakuweza kulenga mpaka Marekani. Wizara ya ulinzi ya Korea kusini pia imesema jeshi la nchi yake na Marekani wanashirikiana katika kubadilishana taarifa za kijasusi kufuatia hatua hiyo ya Korea Kaskazini.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga