1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea kaskazini yafyatua Makombora zaidi.

Halima Nyanza26 Mei 2009

Korea Kaskazini imekaidi shutuma zilizotolewa dhidi yake kimataifa, kutokana na jaribio lake lililofanya la kombora la nyuklia, ambapo leo imefyatua tena makombora ya masafa mafupi huku ikiilaumu Marekani kwa uhasama.

https://p.dw.com/p/HxTu
Kiongozi wa Korea Kaskazini, ambaye nchi yake imekaidi shutuma zilizotolewa kimataifa kwa kufanya jaribio lake la jana la nyuklia, ambapo leo tena imefyatua makombora mengine ya masafa mafupi.Picha: AP

Jeshi la Korea kaskazini leo limefyatua makombora yake mawili ya masafa mafupi, katika eneo la mashariki mwa pwani ya nchi hiyo, siku moja tu baada ya kufanya jaribio lake la kombora la nyuklia ambalo linashutumiwa kimataifa na kuilaumu Marekani kupanga njama dhidi ya serikali yake.


Makombora hayo yalikuwa na masafa ya karibu kilomita 130.

Jana nchi hiyo pia ilifyatua makombora matatu ya masafa mafupi.


Aidha, katika hali ya kuongeza wasiwasi zaidi katika kanda hiyo, Korea kusini imesema itaungana na hatua zinazoongozwa na Marekani kuzuia meli zinazoshukiwa kubeba silaha za maangamizi, kitu ambacho Korea Kaskazini imeonya kuwa itazingatia kama ni kutangaza vita.


Rais Obama amemuhakikishia Rais wa Korea Kusini Lee Myung-back, msimamo wa nchi yake kwa ulinzi wa nchi hiyo.


Jaribio la jana la kombora la nyuklia, ambalo ni la pili kufanywa na Korea Kaskazini baada ya lile la mwaka 2006, lilizua karipio kutoka mataifa ya kanda hiyo, huku Rais wa Marekani Barack Obama akisema mpango huo wa silaha za Atomic unatishia usalama kimataifa.


Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshutumu jaribio hilo la Korea kaskazini na kwamba sasa linafanyia kazi azimio jipya dhidi ya nchi hiyo.

Lakini hata hivyo watafiti wa mambo wanasema China . jirani mkubwa wa Korea kaskazini haielekei kuunga mkono hatua yoyote kali dhidi ya nchi hiyo.


China inaamini kutaka kuirudisha Pyongyang katika mazungumzo ya kanda kwa ajili ya kuachana na mpango wake wa kuwa taifa lenye nguvu za nyuklia.


China na Korea kusini pia zinawasiwasi na hatua itakayochukuliwa dhidi ya jirani yao huyo ambayo inaweza kuyumbisha kwa kiasi kikubwa utawala wa Korea kaskazini na kusababisdha ghasia katika maeneo ya mipaka.


China na Korea kusini na washirika wakubwa wa biashara wa Korea kaskazini, ambapo pato la mwaka linakadiriwa kufikia dola bilioni 20.


Wakati huohuo Mawaziri wa Ulinzi wa Korea kusini na China wanakutana katika mkutano wa usalama ambapo suala la jaribio la nyuklia la Korea kaskazini ndio litakalokuwa ajenda kubwa ya mazungumzo.


Waziri wa Ulinzi wa Korea kusini amewasili tayari mjini Beijing kwa mazungumzo na mwenziye Jenerali Liang Guanglie.



Mwandishi: Halima Nyanza(DPA/AP/Reuters)

Mhariri:M.Abdul-Rahman