Korea Kaskazini yachelea kukishambulia kisiwa cha Guam | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.08.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Korea Kaskazini yachelea kukishambulia kisiwa cha Guam

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong- Un amesema kuwa atasitisha kwa muda mpango wake wa kukishambulia kwa makombora ya masafa marefu kisiwa kinachomilikiwa na Marekani cha Guam kilichoko katika Bahari ya Pasifiki.

Baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa matamshi hayo ya rais wa Korea Kaskazini yanafungua njia katika kuelekea kupunguza makali ya mgogoro uliopo kati ya pande hizo mbili unaochochewa na vita vya maneno kati ya Rais Donald Trump na Kim Jong Un.

Vita vya maneno vya hivi karibuni kati ya viongozi hao vilisababishwa zaidi na kitisho cha Korea Kaskazini cha kutaka kufyatua makombora manne kuelekea Japan na hadi katika kisiwa cha Guam, ambalo ni eneo maalumu kimkakati kwa ajili ya ulinzi kwa Marekani.

Shirika la habari la Korea Kaskazini, KCNA, limeripoti kuwa kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un, alifahamishwa   juu ya mpango wa kukishambulia kisiwa cha Guam kwa makombora, wakati alipokagua kikosi maalumu kinachohusika na mashambulizi ya makombora ya masafa marefu. Hata hivyo, kiongozi huyo alisema atasubiri kwanza kidogo hadi atakapoona kile alichokiita "upumbavu na ujinga wa Marekani."

 Amekaririwa akisema kuwa iwapo Marekani wataendelea na uchokozi wao katika Rasi ya Korea, basi Korea Kaskazini italazimika kuchukua hatua kama alivyokwishasema hapo kabla.

Ameongeza kuwa ili kupunguza makali ya mvutano huo na kuzuia hatari iliyopo ya mashindano ya silaha za kijeshi  katika Rasi ya Korea, basi ni lazima Marekani itumie njia ambazo zitaepusha hali hiyo.

Matamshi ya Kim Jong Un yanaonekana kugusia juu ya mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Korea Kusini na Marekani yanayofanyika kila mwaka na ambayo yanatarajiwa kuanza baadaye mwezi huu.

Hata hivyo, Marekani na Korea Kusini zinasisitiza kuwa mazoezi yao ya pamoja ya kila mwaka ni ya kujilinda tu na hayapaswi kuhusishwa na mpango wa makombora wa Korea Kaskazini, ambao unakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Tangazo la Korea Kaskazini la kusimamisha hatua zake za kijeshi ilizokuwa imelenga dhidi ya kisiwa cha Guam zimeibua furaha katika kisiwa hicho, ambapo maafisa wa eneo hilo wamesema ni ishara kuwa Kim Jong Un amelazimika kubadili msimamo wake.

Trump tayari amekwishaionya Korea Kaskazini

US-Präsident Donald Trump (Reuters/J. Ernst)

Rais Donald Trump wa Marekani

Mvutano kati ya Korea Kaskazini na Marekani umeshika kasi katika siku za hivi karibuni tangu Korea Kaskazini ilipofanya majaribio mawili ya makombora ya kutoka bara moja kwenda jingine ambayo yalioneka zaidi kuilenga Marekani, hatua iliyopelekea Rais Trump kuionya Korea Kaskazini, akisema atachukua hatua kali za kijeshi ambazo dunia haijawahi kuzishuhudia, huku nayo Korea Kaskazini ikijibu kuwa iwapo hilo litatokea, basi itakishambulia kisiwa cha Guam kilichoko katika bahari ya Pasifiki kinachomilikiwa na Marekani.

Mzozo huo umeigusa dunia ambapo viongozi wa baadhi ya mataifa yenye nguvu duniani ikiwa ni pamoja na Rais Xi Jinping wa China wametoa mwito wa  pande zote mbili kupunguza makali ya mvutano uliopo.

Hayo yanatokea huku China ikitangaza kuanzia leo kuchukua hatua za kuzuia bidhaa kutoka Korea Kaskazini yakiwemo makaa ya mawe na samaki, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Umoja wa Mataifa la hivi karibuni dhidi ya Korea Kaskazini ambayo ni mshirika wake kibiashara.

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com