Kombe la UEFA:Shakhtar Donetsk 2:Bremen 1 | Michezo | DW | 21.05.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la UEFA:Shakhtar Donetsk 2:Bremen 1

Mabingwa wapya wa UEFA CUP ni Shakhtar Donetsk ya Ukraine.

default

Shakhtar's Doneck Dario Srna.

Mabingwa wapya wa Kombe la ulaya la UEFA ni Shakhtar Donetsk ya Ukraine ilioizaba jana Werder Bremen ya Ujerumani mabao 2:1 katika finali ya Kombe hilo mjini Istanbul,Uturuki.Mbrazil Jadson, alilifumania lango la Bremen , dakika 7 baada ya kurefushwa mchezo. Bremen ilionekana dhahiri imewakosa uwanjani mastadi wake 3 mbrazil Diego,mshambulizi Almeida na beki mshahara wa Ujerumani Mertesacker.

Mbrazil Luiz Adriano alilifumania lango la Werder Bremen kwa bao la kwanza mnamo dakika ya 25 ya mchezo,lakini Bremen ikaiambia Donetsk kutangulia si kufika:Naldo akasawazisha dakika 10 tu baadae kupitia m kwaju mkali na maridadi wa (freekick).

Timu hizo mbili zikisimama sare bao 1:1 hadi dakika ya 90 ya mchezo, mpambano ukarefushwa kuamua mzizi wa fitina.Jadson,mbrazil mwengine akatia bao la ushindi la waukraine mnamo dakika ya 7 ya kurefushwa mchezo. hii ikaifanya Shakhtar Donetsk kuwa timu ya kwanza ya Ukraine kutwaa Kombe la ulaya la UEFA ingawa Dynamo Kiev iliwahi kushinda Kombe la washindi la Ulaya-winners cup.

Rais Viktor Yushchenko, wa Ukraine akiwa binafsi uwanjani kujionea finali ya jana,kocha wa Shakhtzar, mrumania Lucescu aliiteremsha timu yake uwanjani akiipa jukumu moja la kuhujumu.Kikosi chake cha mfumo wa 4-4-2 kilijumuisha wabrazil 5 waliohanikiza mara kwa mara katika lango la Bremen.

Tofauti kabisa na mkondo wa mchezo, mshambulizi wa Bremen kutoka Peru, Claudio Pizarro angeweza kuipatia timu yake bao la 2 mnamo dakika ya 78 ya mchezo na kuepuka kurefushwa mchezo,lakini kipa wa Shakhtar -Pyatov alikuwa macho kabisa.

Kocha wa Bremen Thomas Schaaf alisema, " inatubidi kuridhia tumeshindwa na tunaipopngeza Shakhtar kwa ushindi wake.Hatukugundua mchezo wetu."

Mchezaji wa kiungo wa bremen Trosten Frings amesema Bremen sasa inabidi kupumzika na kujiwinda kwa finali ya Kombe la Ujerumani siku 9 kutoka leo mjini Berlin dhidi ya Bayer Leverkusen. Frings akaongeza, "tumevunjika moyo sana ,kwani tulipigana kufa kupona,lakini ,walipotia bao la ushindi hatukua na jibu.

Bremen haina wakati lakini wa kupumua,kwani keshokutwa jumamosi ina miadi na viongozi wa Ligi wa Bundesliga-VFL Wolfsburg katika finali ya timu 3 ya kuania taji-Wolfsburg,Bayern Munich na Stuttgart.Kila moja yaweza kutwaa taji Jumamosi hii.Wolfsburg ikiongoza Ligi kwa pointi 2 mbele ya mabingwa Munich,inahitaji kutoka sare tu au pointi 1 kutwaa ubingwa.Munich inabidi kutumai Bremen inaishinda Wolfsburg na wao wanailaza Stuttgart kwa mabao alao 7.Ishara zote zaonesha Bremen kama jana usiku ilipoitawaza Shakhtar Donets mabingwa wa UEFA, Jumamosi hii watakuwa farasi wa kupanda kwa Wolfsburg kutwaa ubingwa.

Muandishi:Ramadhan Ali/DPAE

Mhariri:M.Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com