Kombe la klabu bingwa Afrika | Michezo | DW | 08.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la klabu bingwa Afrika

Al Ahly ya Misri ina miadi na etoile du sahel ya Tunisia kwa finali yake ya 3 mfululizo ya kombe la klabu bingwa. Wakenya na waethiopia watamba katika Cologne na Chicago marathon.

Munich na Nüremberg uwanjani

Munich na Nüremberg uwanjani

Mabingwa wa Afrika Al Ahly(Misri),wameingia finali yao ya 3 mfululizo ya kombe la klabu bingwa lakini walihitaji bao la sadaka kutoka kwa mahasimu wao Al Ittihad ya Libya kuondoka na ushindi mjini Cairo.

Mlinzi wa Al Ittihad Shaban alikosea na kuutia mpira kichwa ulioongoza hadi langoni mwake akijaribu kuokoa.Mkasa huu ulitokea mnamo dakika ya 20 ya mchezo na Al Ahly ikalizuwia bao hilo lisiwaponyoke hadi firimbi ya mwisho.

Sasa Al Ahly wanakumbana na Etoile du sahel ya Tunisia katika finali ya kombe hili la klabu bingwa .Etoile iliitimua Al Hilal ya Tunisia nje ya kombe hilo kufuatia ushindi jumla wa mabao 4-3.Al Ahly inatapia kuwa timu ya kwanza kunyakua kombe hili la klabu bingwa kwa mwaka 3 mfululizo.Wakati huo huo ikilitwaa itaweka rekodi ya ushindi wake wa 6.

Kinyan’ganyiro cha mwaka huu cha Kombe la CECAFA (Challenge Cup)kwa Afrika mashariki na kati kitachezwa Tanzania kuanzia Desemba 8 hadi 22. Super Eagles,timu ya taifa ya Nigeria-chini ya kocha Berti Voigts huenda ikawa na changamoto ya kirafiki na Taifa Stars mjini Dar-es-salaam.

Katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani,mtaliana Luca Toni, aliufumania mara mbili mlango wa Nüremberg jana kuipa Bayern Munich uongozi wa pointi 5 kileleni mwa Bundesliga.Toni alipiga hidi langoni mwa Nüremberg mnamo dakika ya 31 baada ya mkwaju wa Hamit Alintop.Ze Roberto wa brazil akatia bao la 3 la Munich.

Maajabu mwishoni mwa wiki yamezushwa na klabu chipukizi ya Karlsruhe,ilioparamia kileleni hadi nafasi ya pili nyuma ya Bayern Munich.Karlsruhe iliitandika Schalke 04 hapo jumamosi mabao 2:0.Mabao yote 2 yalikomewa wavuni na Tim.

Je, Karlsruhe sasa ina azma ya kufuata nyayo za Kaiserslauten-klabu iliopanda daraja ya kwanza kutoka ya pili na msimu huo huo kutwaa ubingwa?

Kocha wa Karlsruhe anasema, la,hasha.

“Swali la ubingwa kwetu sio mada yetu.Azma yetu ni kubakia katika daraja ya kwanza ya Bundesliga na kwa ushindi huo wa mabao 2:0 hii leo tutaendeleza hapo kwenda mbele.”

Katika mashindano ya mwaka huu ya Cologne-marathon hapa Ujerumani,wakenya 2 walinyan’ganyia ushindi kati yao:Mwishoe, Daniel Too alimpiku Samuel Muturi kunyakua ushindi kwa muda wa masaa 2:11:05.Nafasi ya 3 pia ilienda Kenya kwa Benjamin Itok.

Upande wa wasichana, ushindi ulibakia Ujeruimani:Sabrina Monckenhaupt kutoka jiji la Cologne,aliwapiku wasichana wakenya na waethiopia na mwishoe kuibuka mshindi.Nafasi ya pili alifuata Susanne pumper wa AUSTRIA WAKATI MUETHIOPIA Worknesh Tola akibidi kuridhika na nafasi ya 3.Mashindano ya Cologne marathon yanafuatia yale ya wiki moja kabla ya Berlin marathon ambamo Muethiopia Haile Gebrselassie aliivunja rekodi ya dunia ya mkenya Paul Tergat.

Katika Chicago marathon ushindi upande wanaume ulinyakuliwa n a mkenya Patrick Ivuti aliemkimbia jana mmorocco Jaouad Gharib.Ivuti na Gharib walikuwa bega kwa bega wakivuka mstari wa mwisho.Muda wa mshindi Ivuti ulikuwa masaa 2:11.11 sek.Mkenya Daniel Njenga alimaliza nafasi ya tatu.

Upande wa wanawake, ushindi ulienda kwa mwanariadha mkongwe wa Ethiopia, Berhane Adere.

Kila mmoja kati ya Patrick Ivuti na Adere, ameondoka na kitita cha dala 125,000.

RUGBY: kombe la dunia la rugby Ufaransa:

Afrika kusini na Argentina zilikata jana tiketi zao za nusu-finali ya kombe hilo la dunia.Springboks, amabao sasa wanapigiwa upatu kutwaa tena ubingwa tangu 1995 baada ya kutimuliwa nje Australia na New Zealand, watatolewa hata hivyo jasho na Argentina.

Argentina imefika mara ya kwanza kabisa nusu-finali ya kombe hili.Wakati Afrika kusini imeitimua Fiji kwa mabao 37-20, Argentina imeipiga kumbo Scotland .Nusu-finali ya pili itakua kati ya mabingwa Uingereza na wenyeji Ufaransa.

 • Tarehe 08.10.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7nY
 • Tarehe 08.10.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7nY