1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Afrika

29 Januari 2008

Hatima ya Kamerun kucheza duru ijayo yaamuliwa leo huku mabingwa Misri wakiumana na Zambia .

https://p.dw.com/p/CzIX

Katika kinyan’ganyiro cha kombe la Afrika la mataifa, Otto Pfister,kocha wa kijerumani ambae simba wa nyika-kamerun hawakumtaka,anaweza leo kuwaongoza kukata tiketi yao ya duru ijayo ya robo-finali. Simba wa nyika wana miadi leo na mamba wa mto nile-Sudan wanaoburura mkia wa kundi C.

Katika mpambano wapili mjini Kumasi, mabingwa Misri wameahidi kutoregeza kamba watakapocheza leo na Chipolopolo-Zambia katika uwanja wa baba Yara stadium mjini Kumasi.

Misri tayari wana pointi 6 kutoka mechi 2 walizocheza.Kwanza waliikandika kameroun mabao 4:1.

Misri-mabingwa hadi sasa wametia mabao 7 katika mapambano 2 na leo hawakusudii kamwe kupunguza kasi.Kocha wao Hassan Shehata amesema,

„Tumekuja hapa kushinda na jukumu letu kama mabingwa ni kubwa zaidi kuliko la timu nyengine .“

Shehata akaongeza ingawa tumeshinda mechi zetu 2 za kwanza,bado hatujatia mfukoni tiketi ya robo-finali na hivyo tumejiwinda kwa mpambano na Zambia.

Kocha wa Misri amesema kombe hili la Afrika hakuna timu hafifu na timu nyingi na hirimu sawa.Angalia Angola ilivyoitoa Senegal.

Misri ilitawazwa mabingwa wa Afrika lilipoasisiwa kombe hili mjini Khartoum, Sudan, 1957,halafu tena nyumbani cairo, 1959,na tena nyumbani 1986,1998 huko Burkina Faso na nyumbani 2006.Jinsi Misri ilivyotamba katika kombe hili la Afrika inatoa ishara zaidi hata kuliko 2006 nyumbani kwamba wanaweza kurudi cairo na kombe la 6 la Afrika.

Zambia kwa upande wake inasikitika kwa madhambi mngome yao iliofanya ilipocheza na simba wa nyika-Kamerun mpambano uliopita.

„Ulinzi ndio nguvu kubwa ya timu ya zambia ,lkini kwa mara ya kwan za ilivuja na Kamerun imetumia nafasi hiyo kutia magoli.“ Alisema Patrick Phiri.

Mabingwa mara 4-Kamerun wakiongozwa na kochya wao mjerumani Otto Pfister,walilipiza kisasi chao cha kuzabwa mabao 4-1 na mabingwa Misri kwa kuionea Zambia kwa mabao 3-0.Kamerun inaongozwa katika changamoto ya leo na mjerumani Otto Pfister mwenye umri wa miaka 70 anaeiamini aweza kuirejesha kamerun kileleni mwa dimba la afrika.

Jogoo la Kamerun,Samuel Eto’o lina uchu leo wa kuvunja rekodi ya mabao 14 alioiweka Laurent Pokou wa Ivory Coast.Dhidi ya zambia, Eto’o alisawazisha rekodi hiyo na ikiwa leo atawika ,rekodi ni yake.

Kama jana pale kocha mwengine mjerumani Berti Vogts hatima yake ilitegemea ushindi dhidi ya Benin, hatima otto Pfister,yaweza pia ikaamuliwa na mpambano huu.

Hapo kabla, Otto Pfister,kocha mkongwe kabisa kati ya wote waliopo Ghana,alikuwa Sudan akiongoza klabu ya Al-Merreikh,huko Oumduraman.Aliitawaza klabu hiyo mabingwa wa kombe la CAF-kombe la shirikisho la dimba la afrika mwaka uliopita.Baadae akaiacha mkono kuwaongoza simba wa nyika katika kombe hili la Afrika nchini Ghana.Ishara zote zaonesha Kamerun licha ya kuteleza,inasonga mbele alao katika duru ijayo.