Kombe la Afrika laingia awamu ya mtoano | Michezo | DW | 30.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la Afrika laingia awamu ya mtoano

Guinea yaingia robo fainali na inapimana nguvu na Ghana siku ya Jumapili, wakati wenyeji Guinea ya Ikweta ina miadi na Tunisia na Algeria itaoneshana kazi na Cote D'Ivoire katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika.

2015 Afrika Cup Gruppe D Guinea Fußballmannschaft

Timu ya taifa ya Guinea

Kigogo kimoja kinachopigiwa upatu kutoroka na taji la kombe la mataifa ya Afrika mwaka huu kitalazimika kuaga mashindano hayo wakati Algera na Cote D'Ivoire watakapokutana katika robo fainali ya mashindano hayo kesho Jumapili.

Afrika Cup Tunesien vs Sambia 22.01.2015

Wachezaji wa Tunisia

Pambano hilo la kesho Jumapili(01.02.2015) mjini Malabo kati ya timu mbili zilizoshiriki katika fainali za kombe la dunia mwaka jana ni mchezo unaoangaliwa kwa karibu na wadadisi na wapenzi wa michezo barani Afrika miongoni mwa timu nane zilizofanikiwa kuingia katika robo fainali wakati michuano hiyo ya wiki tatu ikiingia katika awamu ya mtoano leo Jumamosi.

Ghana , kikosi kingine miongoni mwa timu za Afrika iliyoshiriki katika fainali za kombe la dunia nchini Brazil miezi sita iliyopita , inaumana na Guinea mjini Malabo mapema siku ya Jumapili.

Fußball Afrika Cup of Nations Kongo vs. Gabon 21.01.2015

Wachezaji wa timu ya Congo Brazzaville

Leo Jumamosi(31.01.2015) , wenyeji wa mashindano hayo Guinea ya Ikweta itawania kuendeleza ndoto yao wakati itakapokabiliana na Tunisia mjini Bata baada ya pambano la watani wa jadi baina ya Congo Brazzaville dhidi ya jamhuri ya kidemokrasi ya Congo .

Africa Cup Fans

Mashabiki wa kandanda katika michuano ya kombe la Afrika

Michezo ambayo ilikuwa ifanyike katika miji midogo ya upande wa mashariki ya Ebebiyin na Mongomo imehamishwa kutokana na hofu ya usalama pamoja na hali ya viwanja pia.

Algeria , timu inayoongoza katika orodha ya FIFA kwa timu za Afrika , imeendelea kuonesha mafanikio katika miezi 12 iliyopita, ikiwa ni pamoja na kuilazimisha Ujerumani ambayo ni mabingwa wa dunia kuingia katika muda wa nyongeza katika mchezo wao wa kombe la dunia.

Tangu wakati huo ushindi mara tano katika michezo sita katika michezo ya kufuzu kuingia katika fainali za kombe la Afrika imefuatiwa na ushindi katika awamu ya makundi dhidi ya Afrika kusini na Senegal.

Interaktiver WM-Check 2014 Mannschaft Elfenbeinküste

Kikosi cha tembo wa Cote D'Ivoire

Wakati tukiwa hewani Congo Brazzaville imo uwanjani kupambana na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, na baadaye Tunisia itaoneshana kazi na wenyeji Guinea ya Ikweta.

Kombe la mataifa ya Asia

Katika kombe la mataifa ya Asia , Australia ina lenga kulinyakua kombe hilo kwa mara ya kwanza leo Jumamosi , lakini kushindwa ama kushinda , kocha Ange Postecoglou anaamini walivyocheza katika mashindano hayo kutasaidia kuendeleza kandanda nchini humo.

Australia iko ukingoni mwa kulinyakua taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo lakini kabla ya mchezo huo kocha Ange Postecoglou anaangalia hali pana zaidi.

Asian Cup Fußball Australien 2015

Wachezaji wa Australia

"Tunaangalia kuhusu mchezo wenyewe tu" kile kitakachotokea hapo baadaye ni muda tu utaamua , Postecoglou amewaambia waandishi habari. Fahari yangu inakuja kutokana na ukweli kwamba mchezo wa kandanda katika nchi hii umepata msukumo mkubwa mwezi huu.

Australia ilijiunga na shirikisho la kandanda la mataifa ya Asia mwaka 2006 baada ya kuwa timu ambayo inashinda bila kikwazo kila mara katika shirikisho la mataifa ya bahari, Ocean na Postecoglou anaamini hata Australia ikishindwa katika fainali na Korea ya kusini haitazuwia kuendelea kwa mchezo huo.

Moyes katika mtihani na Real

David Moyes atakabiliana na mtihani wake mkubwa tangu kuanza kuifunza timu ya Real Sociadad wakati kikosi hicho kutoka jimbo la Basque kinaizuru Real Madrid uwanjani Santiago Bernabeu leo Jumamosi jioni.

Asian Cup Fußball Korea Irak

Wachezaji wa Korea ya kusini wakishangilia bao

Hata hivyo , ziara hiyo ya kikosi cha David Moyes sio ngumu hivyo kama ingekuwa yupo mchezaji bora wa dunia mara tatu Cristiano Ronaldo ambaye anatumikia adhabu baada ya kumshambulia mlinzi wa timu ya Cordoba Edimar katika mchezo ambao Madrid ilishinda mwishoni mwa juma kwa mabao 2-1.

Michezo mingine ni pamoja na Eibar inapambana na Atletico Madrid , Granada inaikaribisha nyumbani Elche na celta Vigo iko nyumbani ikiisubiri Cordoba.

FC Everton Trainer David Moyes

Kocha wa Real Sociedad David Moyes

Kesho Jumapili Levante itaumana na Athletic Bilbao, Almeida na Getafe , Sevilla inaoneshana kazi na Espanyol na Barcelona itakuwa nyumbani ikiisubiri Villareal.

Copa del Rey

Wakati huo huo Villareal itapambana katika nusu fainali ya kombe la mfalme Copa Del Rey nchini Uhispania dhidi ya Barcelona baada ya Villareal kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Getafe siku ya Alhamis wiki hii na kupata jumla ya mabao 2-0 katika michezo miwili ya kombe hilo.

Espanyol pia inasonga mbele katika nusu fainali kwa kuishinda Sevilla kwa jumla ya mabao 3-2 , ambapo itakwaana na Athletic Bilbao katika nusu fainali. Barcelona imeingia katika duru hiyo kwa ushindi jumla wa mabao 4-2 dhidi ya Atletico Madrid.

Fußball Chelsea Andre Schürrle

Andre Schuerrle anayehamia Wolfsburg kutoka Chelsea

Kwaheri Chelsea

Na katika Bundesliga, wolfsburg imepata saini ya mshambuliaji wa pembeni wa timu ya taifa ya Ujerumani Andre Schuerrle akitokea Chelsea ya mjini London kwa kitita kinachoripotiwa kufikia kiasi cha euro milioni 30.

Mkurugenzi mkuu wa Wolfsburg Klaus Allofs amethibitisha kwamba klabu hiyo ya Bundesliga ilikuwa inafanya majadiliano kupata saini ya mshambuliaji huyo wa pembeni mwenye umri wa miaka 24 lakini imesema jana Ijumaa kuwa mambo bado hayajakamilika.

Wolfsburg hata hivyo iko tayari kumwachia mshambuliaji kutoka Croaria Ivica Olic ambaye tayari yuko mjini Hamburg kwa ajili ya uchunguzi wa kiafya na klabu ya SV Hamburg.

Junentus Turin inakabiliwa na mchezo ambao huenda ukawa mgumu kesho Jumapili wakiwania kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi ya Italia Serie A na kuendeleza pengo la pointi saba wakati watakapopambana na Udinese , wakati mpambano wa kuwania nafasi ya tatu na ya mwisho ya kucheza katika champions League unaingia katika hatua yake ngumu.

Leo jioni Genoa itapambana na Fiorentina , Roma itakwaana na Empoli. Kesho Jumapili ni zamu ya Sassuolo ikiikaribisha Inter Milan , Atalanta inaoneshana kazi na Cagliari, Cesena ina kibarua na Lazio , Chievo wanaikaribisha Napoli, Parlemo inaumana na Verona, na Milan iko nyumbani ikiisubiri Parma.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre

Mhariri: Saumu Mwasimba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com