Kombe la Afrika-Ghana | Michezo | DW | 28.01.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la Afrika-Ghana

Kocha wa Simba wa Teranga, Senegal mpoland Henri Kasperczak ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo muda mfupi baada ya timu hiyo kupata kipigo cha kushangaza cha mabao 3-1 kutoka kwa Angola hapo jana.

default

Mmoja wa washabiki wa Angola akishangilia ushindi wa timu yao ya Taifa

Matokeo hayo yameifanya Senegal kuwa katika ncha ya kuziaga fainali fainali hizo pasipokutegemea mechi yao ya mwisho dhidi ya afrika kusini siku ya alhamisi.


Angola na Tunisia zina pointi nne kila mmoja na zinahitaji sare tu zitakapokumbana kuweza kufuzu kutoka katika kundi lao.


Sasa Simba hao wa Terenga watakuwa chini ya kocha msaidizi Lamine Ndiaye.


Senegal ikiwa na wachezaji karibu wote wanaosukuma ngozi ya kulipwa barani Ulaya ilikuwa ikipigiwa upatu kufuzu kutoka katika kundi hilo, lakini pointi moja iliyokuwa nayo mpaka sasa inaifanya safari yao ya kurudi Dakar kuiva.


Kipigo cha hapo jana kutoka kwa Angola ambayo ni wenyeji wa fainali zijazo za afrika mwaka 2010, kiliwafanya washabiki wa Senegal nyumbani Dakar kufanya ghasia na vurugu mitaani wakishindwa kuamini kile walichokiona katika runinga.


Leo hii Morocco inaingilia na wenyeji Ghana, ambapo ili iwe katika nafasi ya kufuzu inatakiwa kuwafunga wenyeji hao.


Ghana wenye pointi sita mpaka sasa wanahitaji sare tu kuweza kuwa na uhakika wa kucheza robofainali, na kuwaachia Morocco na Guinea uwanja wa kuwania nafasi ya pili.Zote zina pointi tatu, kila mmoja.


Hata hivyo kiwango kilichooneshwa na Ghana katika mechi mbili zilizopita kinawakatisha tamaa washabiki wao.


Hata kiungo wa timu hiyo Michael Essien amesema kuwa ni dhahiri wanatakiwa kukaza kisuli hii leo ili kushinda mechi hiyo.


Kiwango hicho kimewafanya washabiki wa Ghana kutoa vitisho kwa wazazi wa wachezaji wawili wa timu hiyo mshambuliaji Asamoha Gyan na kaka yake Baffour.


Kitendo hicho kiliwafanya wachezaji hao watake kujitoa kwenye timu hiyo hapo jana na ilimbidi kocha wa timu hiyo mfaransa Claude Le Roy kuwabebembeleza.

Kwa upande wao Guinea wanaonekana kuwa katika nafasi angalau rahisi kwani wanapambana na timu dhaifu katika kundi hilo Namibia


Tayari kuna shtuma ya kwamba wachezaji wa Namibia wamefuatwa kuahidiwa mlungula yaani rushwa ili kupoteza mechi hiyo.


Rais wa chama cha soka cha Namibia Pascal Feindouno amesema kuwa wachezaji walifuatwa na mtu mmoja mcheza kamari kutoka Asia na kuwaahidi kitita cha fedha cha dola elfu 30 kila mmoja ili kuachia mechi hiyo ya leo dhidi ya Guinea.


Mapema kabla ya hapo Kocha wa Benin Mjerumani Reinhard Fabisch alidai kufuatwa na mtu huyo na kumtaka kufanya udanganyifu katika mechi ya Benin dhidi ya Mali.Benin tayari imekwishaziaga fainali hizo.


Lakini afisa mmoja wa shirikisho la soka la Afrika CAF Soulemine Hubouba amesema kuwa Shirikisho hilo linayafanyia uchunguzi madai hayo.


Katika hatua nyingine Shirikisho hilo la soka la Afrika limempatia onyo kali kiungo wa mabingwa watetezi Misri Mohamed Aboutrika kutokana na kitendo chake cha kushangalia kwa kuonesha ishara ya kisiasa.


Farau huyo Aboutrika alivua jezi yake baada ya kupachika bao katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0 dhidi ya Sudan, ambapo ndani kulikuwa na fulana yenye maandishi ya kuwaunga mkono wapalestina katika madhila wanayokabiliana nayo huko Gaza.


Kwa ujumla mpaka sasa fainali hizo zimeshuhudia mabao 54 yakipachikwa wavuni, huku Misri na Ivory Coasta zikiwasisimua washabiki kwa kandanda lao


Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com