1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Koeman: Messi aheshimiwe zaidi

1 Februari 2021

Kocha wa miamba wa kandanda nchini humo Barcelona Ronald Koeman amesema Lionel Messi anastahili kuheshimiwa zaidi baada ya tukio la kandarasi yake kuvujishwa.

https://p.dw.com/p/3ofgT
Lionel Messi
Picha: Imago Images/ZUMA Wire/E. Alonso

Hapo Jumapili Barcelona ilisema inaweza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya gazeti la Uhispania El Mundo baada ya gazeti hilo kuchapisha taarifa kuhusiana na kandarasi ya mchezaji huyo.

Katika taarifa klabu hiyo imesema inasikitishwa na tukio hilo ukizingatia kuwa kandarasi ni waraka wa siri kati ya pande mbili zinazohusika. Na sasa Koeman anataka kuwepo na heshima zaidi.

"Kilichotokea katika vyombo vya habari kusema kimefanyika kwa nia mbaya na lengo ni kumuumiza mchezaji ambaye tunastahili kumheshimu sana, ni mtu ambaye amechangia mengi kwa kandanda la Uhispania na klabu hii. Leo hii ameonya kwa mara nyengine kwamba yeye ni mshindi, kwa kuwa akili yake aliiweka kwenye mechi tu licha ya yote yaliyotokea," alisema Koeman.

Messi ambaye amesema anatafakari kulishtaki gazeti hilo la El Mundo, alifunga goli maridadi Jumapili kupitia mkwaju wa frikiki Barca walipokuwa wakicheza na Athletic Bilbao katika La Liga, ambapo walishinda mechi hiyo 2-0 Antoine Griezmann akifunga bao la pili.