1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Klitschko kupanda ulingoni dhidi ya Fury

27 Novemba 2015

Tyson Fury anakabiliwa na mtihani mgumu baada ya kudai kuwa atauwekea kikomo utawala wa miaka minne wa Wladmir Klitschko kama bingwa wa ulimwengu bila kupingwa wa uzani wa heavyweight

https://p.dw.com/p/1HDko
Boxsport Schwergewicht Wladimir Klitschko und Herausforderer Tyson Fury
Picha: picture-alliance/dpa/R. Vennenbernd

Mabondia hao wawili watapanda ulingoni mjini Düsseldorf Ujerumani kwa pigano la taji la ulimwengu.

Muingereza huyo mwenye umri wa miaka 27 hajashindwa katika mapigano 24 huku akishinda 18 kwa njia ya knockout, na anakutana na bingwa aliye na uzoefu mkubwa, anayemshinda umri kwa miaka 12 na anayeshikilia mikanda ya WBA, IBF, IBO na WBO. Fury amesisitiza kabla ya pigano hilo kuwa atamnyamazisha Klitschko ulingoni "Nini kinanifanya nifikirie hilo? Kwa sababu mimi ndiye kimbunga. Tyson ni mwenye kasi na ghadhabu! Sijawahi kushindwa na sitashindwa leo usiku. Hiyo ni kwa sababu wapinzani wote wa nyuma walikuja hapa Ujerumani wakiamini kuwa watashindwa. Walikuwa hapa kwa ajili ya pesa. Pesa sio motisha yangu. Kushinda ndio motisha yangu. Na naamini kutoka moyoni kuwa nitashinda pigano hili. Na sio kushinda tu, nitashinda kwa mtindo wa aina yake. na nitaimba wimbo ili kusherehekea ushindi huo"

Klitschko mwenye umri wa miaka 39, aliwahi kushindwa mara tatu zaidi ya mwongo mmoja uliopita na anapanga kumfanya Fury kuwa ushindi wake wa 54 kwa njia a knock put na wake wa 65 katika taluma yake. "Ulingoni nitatarajia kila kitu kutoka kwa Tyson Fury. Ameonyesha kuwa anajiamini sana, anataka kuwa bingwa wa ulimwengu, anataka kunirambisha sakafu na wengine wanaamini hilo. Ninaamini Tyson Fury atakuwa hatari sana".

Pigano hilo awali lilipangwa kuandaliwa Oktoba lakini likaharishwa kutokana na maumivu ya nyonga aliyopata Klitschko ambayo sasa yamepoa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/reuters
Mhariri: Josephat Charo