1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiwango cha gesi ya carbon dioxide chaongezeka

Josephat Charo28 Oktoba 2007

Ongezeko la uoto limelinganishwa na treni kuu kuu inayokwenda kwa mwendo wa kinyonga ambayo abiria wake hawajui janga linalowakabili.

https://p.dw.com/p/C7rZ
Kuyeyuka kwa theluji kwa sababu ya ongezeko la uoto duniani
Kuyeyuka kwa theluji kwa sababu ya ongezeko la uoto dunianiPicha: AP

Kutokana na kuyeyuka kwa theluji katika eneo la Arctic msimu wa kiangazi uliomalizika na ripoti kadhaa juma lililopita kwamba bahari na misitu katika nchi za joto inanyonya kiwango kidogo cha gesi ya carbon dioxide inayotolewa angani duniani kote, treni hii kuu kuu inaonekana tayari imeongeza kasi.

Ongezeko la uoto duniani ni swala kubwa katika maisha ya binadamu kwa wakati huu. Si jambo ambalo vizazi vya kesho pekee ndivyo vitakavyolazimika kukabiliana nalo, amesema Ted Scambos, mtafiti wa sayansi katika taasisi ya barafu na theluji mjini Bolder, Colorado nchini Marekani.

Aina ya mazingira yanayonyonya gesi ya carbon dioxide angani yanashindwa na jambo hili linafanyika kwa kasi kubwa kuliko inavyotarajiwa.

Kiwango cha gesi ya carbon dioxide angani kinaongezeka kwa kasi kuliko ukuaji wa uchumi nchini China na India na uchumi wa dunia unavyochangia. Watafiti wameripoti kwamba hii inasababishwa na kukosekana mazingira ya kuinyonya gesi hiyo katika nchi kavu na baharini.

Takriban nusu ya kiwango cha gesi ya carbon dioxide inayotolewa angani na shughuli za binadamu hunyonywa na vitu asili kama misitu, mimea mingine na bahari. Lakini uchunguzi mpya uliofanywa umedhihirisha kwamba utendaji wa vitu hivi umepungua kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha nusu karne iliyopita.

Corin Le Quéré, mtafiti wa hali ya hewa katika taasisi ya British Antarctic Survey, aliliambia shirika la habari la IPS mwezi Mei mwaka huu kwamba pepo kali katika bahari ya kusini zinazosababishwa na ongezeko la uoto zimesababisha kupungua kwa unyonyaji wa gesi ya carbon tangu mwaka wa 1981.

Pepo hizo huvuma katika bahari na kuleta gesi zaidi ya carbon kutoka baharini hadi nchi kavu na hivyo gesi kidogo hunyonywa kutoka angani. Hali hii inazidi kuongeza asidi baharini hivyo kuhatarisha maisha ya viumbe wa baharini. Bahari nazo pia zinakabiliwa na ongezeko la uoto hivyo haziwezi kunyonya gesi ya carbon dioxide.

Maji ya joto kutoka bahari ya kaskazini ya Pacific yanatiririka katika bahari ya Akitiki, na hii ni mojawapo ya sababu kubwa ya kuyeyuka kwa theluji baharini wakati wa msimu wa kiangazi katika eneo la kaskazini la Akitiki.

Kwa mara ya kwanza kabisa kama binadamu anavyoweza kukumbuka, njia ya kaskazini magharibi kutoka bahari ya Atlantiki hadi bahari ya Pacific haikuwa na theluji.

Ingawa theluji katika bahari ya Kaskazini huyeyuka kidogo kila msimu wa kiangazi, msimu huu kuyeyuka kwa theluji kuliongezeka na kufikia kilomita milioni 2.6 mraba, kiwango kikubwa zaidi kuliko viwango vya misimu ya kiangazi iliyopita.

Dunia inakabiliwa na kitisho cha kufikia kiwango kibaya cha uoto kitakachoiweka katika hatari ya kutoweka katika miaka takriban 100 ijayo ikiwa gesi za viwandani hazitapunguzwa angani. Hayo yamebashiriwa na Peter Mayhew wa chuo kikuu cha York nchini Uingereza.

Sio tu viwango vya joto ambavyo vinaongezeka. Mimea inalazimika kukabiliana na viwango vya juu vya gesi ya carbon dioxide.

Wanasayansi katika taasisi ya utafiti ya Smithson huko Panama wameripoti kuna mimea inayokua kwa haraka huku mizabibu ikiwa imeenea kwa asilimia kati ya 50 hadi 100 katika eneo la Amazon.

Lakini kwa bahati mbaya mimea hii inanyonya kiwango kidogo cha gesi ya carbon ikilinganishwa na miti inayokua pole pole katika nchi za joto. Matokeo yake ni kwamba miti itaweza kunyonya kiwango kidogo cha gesi ya carbon na hivyo kuacha kiwango kikubwa angani.

Ted Scambos wa taasisi ya sayansi ya mjini Bolder, Colorado amesema matumaini pekee ni kupungua kwa kiwango kikubwa cha gesi ya carbon angani. Aidha amesema ikiwa mamilioni ya watu duniani watashinikiza viwango vya gesi za viwandani vipunguzwe, mabadiliko yataweza kutokea kwa haraka.