Kipsang avunja rekodi ya dunia ya marathon | Michezo | DW | 29.09.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Kipsang avunja rekodi ya dunia ya marathon

Mwanariadha wa Kenya Wilson Kipsang ameweka rekodi mpya ya dunia katika mashindano ya 40 ya mbio ndefu ya Berlin Marathon kwa kukimbia kwa saa mbili, dakika tatu na sekunde 38 Jumapili (29.09.2013).

Wilson Kipsang Kiprotich wa Kenya mshindi wa mashindano ya Berlin Marathon (29.09.2013).

Wilson Kipsang Kiprotich wa Kenya mshindi wa mashindano ya Berlin Marathon (29.09.2013).

Kipsang mwenye umri wa miaka 31 alipunguza kwa sekunde 15 rekodi iliyowekwa na mwanariadha mwenzake wa Kenya Patrick Makau ambaye alikimbia kwa saa mbili,dakika tatu na sekunde 38 katika mashindano ya mbio ndefu yaliofanyika mjini Berlin hapo mwaka 2011.Makau alilazimika kujitowa katika mashindano haya wiki mbili zilizopita kutokana na kuumia goti

.Kipsang alikuwa nyuma kwa sekunde nne tu ya rekodi yake hiyo wakati aliposhinda mashindano ya mbio ndefu ya Frankfurt mwaka jana.Hiyo ni rekodi ya nane duniani kuwekwa mjini Berlin katika kipindi cha miaka 15 na kujiimarishia sifa ya kuwa mashindano yenye kutowa wakimbiaji wenye kukimbia kwa haraka kabisa duniani.

Kipsang ambaye alishinda Mbio za Marathon za London hapo mwaka 2002 na pia kujinyakulia medali ya shaba katika michezo ya Olympiki amekaririwa akisema katika mahojiano ya televisheni baada ya mbio hizo " Nina furaha sana kwamba nimeshida na kuvunja rekodi ya dunia."

Kahamasishwa na Tergat

Paul Tergat wakati akivuka utepe wa ushindi katika mashindano ya Berlin Marathon.(28.09.2003).

Paul Tergat wakati akivuka utepe wa ushindi katika mashindano ya Berlin Marathon.(28.09.2003).

Amesema kwa kweli alikuwa amehamasishwa na Paul Tergat wakati alipovunja rekodi ya dunia mjini Berlin miaka kumi iliopita na kwamba ana furaha kubwa kuwa katika nafasi ya kuvunja rekodi hiyo katika mbio hizo hizo.

Rekodi ya Tergat mwanariadha wa Kenya ya saa mbili, dakika nne na sekunde 55 aliyoiweka katika mbio za Marathon za Berlin hapo mwaka 2003 ilikuwa ni ya kwanza kuyakinishwa kuwa ni rekodi ya dunia na Shirikisho la Kimataifa la Riadha Duniani (IAAF) ambalo huko nyuma ndio lililokuwa likizitambuwa rekodi bora za marathon duniani.

Rekodi ya dunia iliokuwa ikishikiliwa na Makau ilionekana kuwa iko salama wakati kundi la wakimbiaji waliokuwa wakiongoza mbio hizi walipokuwa nyuma kwa zaidi ya sekunde 20 baada ya kukimbia kilomita 30 lakini waliweza kujaliza upungufu huo wakati wa kilomita tano zilizobakia kumaliza mashindano hayo.

Hali ya mashindano

Washiriki wakianza mashindano ya 40 ya Berlin Marathon mbele ya lango la Brandenburg mjini Berlin. (29.09.2013).

Washiriki wakianza mashindano ya 40 ya Berlin Marathon mbele ya lango la Brandenburg mjini Berlin. (29.09.2013).

Wakati wanariadha watatu wa Kenya walipokuwa wakiongoza mbio hizo Kipsang alifanikiwa kumponyoka mwanariadha mwenzake bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 5,000 Eliud Kipchoge kwenye kilomita 37 kabla ya kuwa mbele kabisa katika kilomita mbili za mwisho.

Licha ya kukimbia katika hali ya hewa yenye ubaridi kidogo na jua likiwa linawaka,Kipsang amesema angeliweza kukimbia kwa haraka zaidi ingelikuwa amejiandaa vyema zaidi na kubakia kwenye hali nzuri na ingelikuwa hakuna upepo mwingi kama ule uliokuweko wakati wa mbio hizo.

Mwanariadha wa Kenya Wilson Kipsang Kiprotich akipiga picha kwenye bango la mashindano ya Berlin Marathon (27.09.2013) mjini Berlin.

Mwanariadha wa Kenya Wilson Kipsang Kiprotich akipiga picha kwenye bango la mashindano ya Berlin Marathon (27.09.2013) mjini Berlin.

Kufuatia ushindi huo Kipsang amejipatia euro 40,000 na euro 50,000 nyengine kwa kuvunja rekodi .

Katika mbio hizo Eliud Kipchoge ameshika nafasi ya pili kwa kutumia saa mbili, dakika nne na sekunde tano na kuboresha rekodi yake binafsi kwa dakika moja na nusu katika mashindano yake ya pili ya marathon,wakati mwenzao mwengine wa Kenya Geoffrey Kipsang ambaye hana uhusiano na Wilson ameshika nafasi ya tatu kwa kutumia saa mbili, dakika sita na sekunde 26.

Wanawake wa Kenya waibuka washindi

Kwa upande wa wanawake aliyekuwa amewekewa matumaini ya kushinda mbio hizo Florence Kiplagat wa Kenya ameshinda kwa kutumia saa mbili,dakika 21 na sekunde 13 ikiwa ni pungufu ya dakika moja na nusu ya rekodi yake bora na mwenzake Sharon Cherop amekuwa wa pili kwa kutumia saa mbili,dakika 22 na sekunde 28.

Mwanariadha wa Ujerumani Irina Mikitenko akifurahia kufuatia ushindi wake wa Berlin Marathon (28.09.2008) mjini Berlin.

Mwanariadha wa Ujerumani Irina Mikitenko akifurahia kufuatia ushindi wake wa Berlin Marathon (28.09.2008) mjini Berlin.

Mjerumani Irina Mikitenko amemaliza wa tatu na kuweka rekodi mpya ya dunia kwa wakimbiaji waliopindukia miaka 40 kwa kutumia saa mbili,dakika 24 na sekunde 54 ikiwa kama dakika pungufu ya rekodi iliowekwa awali.

Mikitenko amekaririwa akisema"Tayari nina umri wa miaka 40 lakini jambo hilo halimaanishi kitu.Nahisi kama vile nina umri wa miaka 20 nikiwa na uzoefu wa miaka 20"

Ishara ya kuanza kwa mashindano hayo ya Jumapili ilitolewa na mshindi mara nne wa mbio hizo Haile Gebrselassie wa Ethiopia ambaye aliweka rekodi ya dunia mara mbili mjini Berlin.

Wakimbiaji wote wanane ambao waliwahi kuweka rekodi ya dunia mjini Berlin walikuwa katika mbio za Jumapili kuwashangilia wakimbiaji 41,120 kutoka nchi 119 wakati wa kuanza kwa mbio hizo.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters/AP

Mhariri : Hamidou,Oumilkher