kiongozi wa upinzani nchini Sudan, Hassan al-Turabi akamatwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

kiongozi wa upinzani nchini Sudan, Hassan al-Turabi akamatwa

Serikali ya Sudan, imemkamata kiongozi wa upinzani Hassan al-Turabi na wameimarisha juhudi za -kuwondoa waasi wa Darfur.

Wanajeshi wa Chad wakiwa katika mpaka kati ya Chad na Sudan.

Wanajeshi wa Chad wakiwa katika mpaka kati ya Chad na Sudan.

Kwa mara nyingine tena waasi hao walijaribu mwishoni mwa wiki kuushambulia mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum, huku milio ya risasi ikisikika katika mji Mkuu huo.

Siku mbili baada ya shambulio kali ambalo halijawahi kutokea lililofanywa na waasi kwenye mji wa Khartoum, hali ya wasiwasi bado inatanda katika mji huo.

Lakini mshangao zaidi ulikuja pale habari zilipoenea juu ya kukamatwa Hassan al-Tourabi. Mwanasiasa huyo amekuwa akiingia na kutoka jela huko Sudan mara kadhaa.

Akijulikana kama mtu aliyekuwa nyuma ya kuanzishwa sheria za Kiislamu katika Sudan hapo mwaka 1983, al-Tourabi pia alikuwa mtu aliyeshabikiwa sana hapo kabla na rais wa sasa, Omar al-Bashir, baada ya rais huyo alipokamata madaraka katika mapinduzi ya mwaka 1989.

Lakini alishindwa katika malumbano ya kisiasa na mwanafunzi wake, na akavuliwa nyadhifa zake zote mwongo mmoja baadae. Tangu wakati huo amekuwa mmoja wapo wa wapinzani wakubwa wa serekali na ametumikia vifungo mbali mbali gerezani au kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani..

Hassan al-Tourabi ni mwenye siasa za itikadi za Kiislamu, na ushawishi wake unasambaa hadi nje ya mipaka ya Sudan. Alichukuwa masomo yake katika vyuo vikuu vya nchi za Ulaya Magharibi, mjini London, na kuchukuwa shahada yake ya udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Sorbonne, Paris, Ufaransa, mwaka 1964.

Anacharaza uzuri lugha za Kiengereza, Kifaransa na Kijerumani, pamoja , bila ya shaka, na Kiarabu. Ujuzi wake wa kuzisarifu lugha hizo umemsaidia kuwa na mawasiliano rahisi na vyombo vya habari vya nje ambapo mara kadhaa ametoa mwito wa kuweko mapinduzi ya kimataifa ya Kiislamu.

Hassan al-Tourabi alizaliwa mashariki ya Sudan , katika mji wa Kassala, mwaka 1932, kutoka kwa wazee walio watu wa dini. Alijifunza Koran kutoka kwa babu yake, mkuu wa Tariqa ya Kiislamu ya wacha Mungu.

Alijiunga na Chama cha Udugu wa Kiislamu, Muslim Brotherhood, aliporejea nyumbani kutoka Ulaya. Miaka ya sabini alikamatwa mara tatu wakati wa utawala wa Rais Jaafar Numayri.

Lakini alipatana na utawala huo na kufanywa mwanasheria mkuu wa serekali hapo mwaka 1979. Alikuwa mtu aliyeushawishi utawala wa Rais Numayri uamuwe kuanzisha sheria za Kiislamu hapo mwaka 1983.

Uamuzi huo ulikuwa ni cheche zilizowasha moto wa uasi katika eneo la Kusini la Sudan amabako wanaishi watu wengi walio wa dini ya Kikristo au dini za kienyeji. Kulizuka vita ambako Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni mbili walikufa kabla ya mkataba wa amani kutiwa saini mwaka 2005.

Baada ya udikteta wa Rais Numayri kuporomoka mwaka 1986, Hassan al-Tourabi alianzisha Chama cha National Islamic Front na akashindwa katika kuwania uchaguzi wa urais. Alijiunga na Omar al-Bashir mwaka 1989 kuipindua serekali iliokuwa imechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, serekali iliokuwa inaongozwa na shemeji yake, Sadeq al-Mahdi.

Hassan Al-Tourabi alijulikana kuwa ndio nguvu iliokuwa hasa nyuma ya madaraka katika Sudan, na akaiongoza nchi hiyo katika njia ya kidini.

Nchi hiyo ikawa mahala pa kukimbilia Waislamu wenye itikadi kali, akiwemo Osama Ben Laden wa mtandao wa al-Qaida, na kupelekea utawala wa nchi hiyo kulaumiwa kwamba ulikuwa unaufadhili ugaidi na Sudan kutiwa na marekani katika orodha ya nchi korofi duniani.

Lakini mwaka 1999, al-Tourabi aliongoza hatua za kupunguza madaraka ya Rais al-Bashir, hivyo kumfanya rais huyo alivunje bunge na kutangaza sheria ya hali ya hatari. Mwaka mmoja baadae al-Tourabi alipinga al-Bashir asichaguliwe tena kuwa rais.

Mwaka uliofuata akakamatwa pamoja na wafuasi wake wengi baada ya chama chake kutia saini mapatano na waasi wa Kusini mwa Sudan. Aliachiwa kutoka kizuizi cha nyumbani Oktoba 2003, lakini aliwekwa kizuizini tena mwezi Machi mwaka uliofuata akituhumiwa kufanya njama ya mapinduzi..

Kukamatwa jana kwa al-Tourabi kulikuja baada ya wapiganaji wa Darfur wa Chama cha JEM kuushambulia mji mkuu wa Khartoum.

Mke wa mmoja wa maafisa waliokamatwa,Israa Mohammed al-Bashir, ameliambia shirika la Habari la Ufaransa-AFP, kwamba wanatambua kuwa wamemkamata pia Hassan al-Turabi na maafisa wengine wanne wa chama hicho na pengine wanaweza kuwa zaidi.

Amesema hakuna sababu zozote zilizotolewa na polisi juu ya sababu za kukamatwa kwa Kiongozi huyo na maafisa wa chama chake.

Hii ni mara ya kwanza kwa waasi hao katika historia ya machafuko hayo ya miongo na miongo kuufikia mji ambao upo karibu na makao ya Serikali ya Sudan.

Afisa mmoja katika Wizara ya Mambo ya nje, Ali Yousif amesema mpaka sasa Vikosi vya usalama vya Sudan vimeshawakamata raia wa Sudan mia tatu na raia wengine wa Chad kufuatia shambulio lililotokea Jumapili.

Aidha Kiongozi msaidizi wa Kundi la JEM, Suleiman Sandal, amesema mashambulizi yao wameamua kuyaondoa Darfur na kuyahamishia katika mji Mkuu.

 • Tarehe 12.05.2008
 • Mwandishi Scholastica Mazula
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DycS
 • Tarehe 12.05.2008
 • Mwandishi Scholastica Mazula
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DycS
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com