1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa TPLF amuonya Abiy kuondoa wanajeshi wake Tigray

Amina Mjahid
1 Desemba 2020

Kiongozi wa kundi la TPLF katika jimbo la Tigray amemtaka Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kuacha wazimu na kuondoa vikosi vyake katika jimbo hilo huku akisisitiza kuwa bado mapambano yanaendelea.

https://p.dw.com/p/3m4R2
Äthiopien l PK - Dr. Debretsion Gebremichael
Picha: DW/M. Haileselassie

Katika mahojiano kwa njia ya simu na shirika la habari la The Associated Press, Kiongozi wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray,  TPLF  Debretsion Gebremichael, amesema bado yupo karibu na mji mkuu wa jimbo la Tigray, wa Mekelle ambao wanajeshi wa Ethiopia siku ya Jumamosi walitangaza kuudhibiti.

Debretsion, amepuzilia mbali tamko la Abiy kujitangaza kushinda vita kati ya vikosi vyake na vile vya serikali akisema mapambano yanaendelea na wanauhakika wa kushinda. Debretsion Gebremichael pia amevishutumu vikosi vya Ethiopia kwa kuendesha kampeni ya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Tigray.

Mawasiliano katika eneo hilo hadi sasa yametatizwa mwezi mmoja baada ya vita kuanza Novemba 4 na hakuna anaejua ni watu wangapi haswa waliouwawa, na imekuwa vigumu kuthibitisha taarifa zozote kutoka pande mbili hasimu. 

soma zaidi: Gebremichael: Bado vikosi vya TPLF vinapambana Tigray

Kiongozi huyo wa TPLF ameendelea kusema kuwa mapigano yanayoendelea ni ya kulikomboa jimbo la Tigray lililo na idadi ya watu milioni 6 na wataendelea kufanya hivyo hadi pale wavamizi watakapoondoka akimaanisha jeshi la serikali kuu ya Ethiopia. Amedai  kuwa vikosi vyake vimewateka wanajeshi wa serikali akiwemo rubani wa ndege ya kivita wanayodai kuidungua juma lililopita.

Hata hivyo alikataa kujibu suali lolote kuhusu taarifa kuwa kundi lake liliushambulia mji mkuu wa Eritrea Asmara huku akimshutumu Waziri Mkuu Abiy Ahmed kushirikiana na Eritrea kuishambulia Tigray, jambo ambalo serikali ya Ethiopia inaendelea kukanusha.

Abiy Ahmed atuhumiwa kuvitenga vikosi vya TPLF

Äthiopien | Premierminister | Abiy Ahmed Ali
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Picha: Michael Tewelde/AFP/Getty Images

Serikali za kila upande zinashutumiana kutokuwa halali baada ya Abiy kutuhumiwa kukitenga chama cha TPLF kilichotawala katika siasa za Ethiopia kwa takriban muongo mitatu kabla ya Abiy kuingia madarakani mwaka 2018.

Kundi la TPLF limeuelezea utawala wa Abiy kama usiokuwa halali uliojaa ubinafsi na wakidikteta. Maamuzi matatu yalilikasirisha kundi la TPLF, lililotawala muungano wa serikali ya Ethiopia kwa takriban miongo mitatu hadi pale Abiy alipoingia madarakani mwaka 2018: Kuungana kwa Abiy na adui wao Eritrea, kuubadilisha muungano wa kikabila na chama kipya cha kitaifa, pamoja na kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu.

Soma zaidi: Abiy Ahmed: Vikosi vya Tigray vijisalimishe ndani ya masaa 72

Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amezungumza kwa njia ya simu na Abiy  kwa mara ya kwanza tangu mapigano yalipoanza mwanzoni mwa mwezi Novemba, na kusisitiza kusitishwa kabisa kwa mapigano na kufanyika mazungumzo kati ya pande hasimu kuutatua mgogoro uliopo ili kulinda maisha ya raia na kufungua njia kwa misaada ya kiutu kufika eneo hilo.

Msemaji wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Antonio Guterres alipokea simu kutoka kwa Abiy siku ya jumapili na katika mazungumzo yao Guterres akasisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binaadamu na mapatano ya kweli yasio na ubaguzi katika taifa ambalo kila mtu lazima ahisi kuheshimiwa na sehemu ya Ethiopia.

Chanzo: afp, reuters