1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Kiongozi wa Kazakhstan aagiza vikosi kupiga riasi bila onyo

Iddi Ssessanga
7 Januari 2022

Vikosi vya usalama vimeonekana kudhibiti hali katika mitaa ya Kazakhstan, huku rais akisema utaratibu wa kikatiba umerejeshwa kwa kiasi kikubwa, baada ya Urusi kutuma vikosi kuzima maandamano yaliotapakaa nchini humo.

https://p.dw.com/p/45FZ5
Proteste in Kasachstan | TV-Ansprache Präsident Toqajew
Picha: Kazakhstan's Presidential Press Service/AP/dpa/picture alliance

Watu kadhaa wameuawa katika makabiliano ya mitaani, huku waandamanaji wakichoma na kupora majengo ya umma kwenye miji kadhaa, katika vurugu mbaya zaidi kuwahi kutokea tangu taifa hilo la Asia ya Kati kujipatia uhuru wake miaka 30 iliyopita.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi, ikinukuu shirika la habari la Interfax, imesema zaidi ya ndege 70 zimetumika kusafirisha wanajeshi wa Urusi nchini Kazakhstan, na walikuwa sasa wanasaidia kudhibiti uwanja mkuu wa Almaty, uliokuwa umetekwa na waandamanaji siku ya Alhamisi.

Soma pia: Vurugu zazuka upya Kazakhstan baada ya Urusi kutuma askari

Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev amesema Ijumaa kuwa aliwaamuru maafisa wa usalama kufyatua risasi bila kutoa onyo endapo vurugu zitaendelea, na kuapa kuwa hakutakuwepo na majadiliano yoyote na waandamanaji, huku akiahidi kuwasambaratisha wale aliowaita majambazi wenye silaha waliovamia nchi yake.

Russland Soldaten der Luftlandetruppen auf Weg nach Kasachstan
Wanajeshi wa Urusi wakisubiri kupelekwa Kazakhstan kusaidia kudhibiti hali ya machafuko.Picha: Russian Defence Ministry/Tass/imago images

"Operesheni ya kupambana na ugaidi imeanza. Vikosi vya usalama vinafanya kazi kwa bidii. Utaratibu wa kikatiba umerejeshwa katika mikoa yote. Serikali za mikoa zinaidhibiti hali," alisema Tokayev.

Tokayev amesema katika hotuba yake iliyorushwa mubashara kupitia televisheni, kwamba hadi majambazi 20,000 walishambulia mji mkuu wa kibiashara wa Almaty na walikuwa wanaharibu mali ya serikali.

Soma pia: Urusi yapeleka wanajeshi Kazakhstan kutuliza vurugu

Amesema vikosi vya kulinda amani kutoka Urusi na mataifa jirani vilikuwa vimewasili kwa maombi ya Kazakhstan, na kwamba vilikuwa nchini humo kwa muda tu ili kuhakikisha usalama.

Tokayev pia amemshukuru kwa kipekee rais Vladmir Putin pamoja na viongozi wa China, Uzbekistan na Uturuki kwa msaada wao katika kuzima uasi huo.

Kasachstan Taldyqorghan Gebäude der Stadtverwaltung nach Feuer
Moja ya majengo ya serikali yaliochomwa moto na waandamanaji mjini AlmatyPicha: Zhanna Etekbaeva/Sputnik/dpa/picture alliance

Chanzo cha vurugu

Vurugu za aina hiyo hazijawahi kushuhudiwa katika taifa hilo lililotawaliwa kwa mkono wa chuma tangu enzi za Nurusultan Nazarbayev mwenye umri wa miaka 81 sasa, ambaye alikuwa ameendelea kushikilia mamlaka makubwa licha ya kuachia madaraka miaka mitatu iliyopita.

Soma pia: Iran, Urusi na Uturuki zakutana Astana juu ya Syria

Maandamano yaliyoanza kama hatua ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta lililoanza siku ya mwaka mpya,  yalipanuka siku ya Jumatano, baada ya waandamanaji waliokuwa wanaimba nyimbo za kumkebehi Nazarbayev, kuvamia majengo ya umma mjini Almaty na miji mingine.

Waandamanaji wanaituhumu familia ya Nazarbayev na washirika wake kwa kujilimbikizia utajiri mkubwa wakati taifa hilo la wakaazi milioni 19 likisalia maskini. Machafuko hayo yamepelea kufungwa kwa mtandao wa intaneti na mabenki mengi kote nchini humo.

Chanzo: Mashirika