1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

230709 Porsche VW

Josephat Nyiro Charo23 Julai 2009

Mlango wazi sasa Porsche kuungana na Volkswagen

https://p.dw.com/p/Ivpl
Wendelin WiedekingPicha: AP

Mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza magari ya Porsche hapa Ujerumani, Wendelin Wiedeking, amejiuzulu baada ya kuiongoza kampuni hiyo kwa miaka 16. Hatua hiyo inatarajiwa kufungua mlango kwa kampuni ya Porsche kuungana na kampuni ya kutengeneza magari ya Volkswagen ya humu nchini.

Baada ya mkutano wa usiku kucha, uliofanyika katika kituo cha utafiti na maendeleo cha kampuni ya Porsche huko Weissach, karibu na mji wa Stuttgart, bodi ya kampuni ya Porsche imetangaza kwamba meneja anayehusika na uzalishaji katika kampuni hiyo, Michael Macht, ataiongoza kampuni hiyo kujaza pengo lilioachwa na kiongozi wa kampuni ya Porsche, Wedeling Wiedeking.

Kilichokuwa kikifahamika tangu awali ni kwamba kampuni ya Porsche ilitaka kutayarisha njia kuweza kuunda kampuni mpya na kampuni ya kutengeza magari ya Volkswagen kwa lengo la kutaka kuondokana na shinikizo la deni lake kubwa. Ndiyo maana bodi ya kampuni ya Porsche imeridhia kutafuta nyongeza ya kiwango cha Euro bilioni 5 na kuyaunga mkono mazungumzo na Qatar.

Muwafaka huo umefikiwa katika mkutano uliofanyika usiku wa kuamkia leo ambapo mazungumzo yametuwama juu ya hatima ya kampuni ya Porsche. Msemaji wa kampuni ya Porsche, Albrecht Bamler, amesema bodi ya magavana inayoisimamia kampuni hiyo imekubali kutiliana saini na Qatar, ambayo imekuwa ikiendelea kufanya mazungumzo na kampuni hiyo ya Porsche. Hata hivyo, msemaji huyo hakusema ikiwa Euro hizo bilioni 5 zitatoka Qatar, kwa muwekezaji mwingine, kwa familia inayoimiliki kampuni ya Porsche au ni fedha zilizoongezwa juu ya kiwango cha awali kilichotakiwa kutolewa na Qatar.

Bila shaka, fedha hizo zitaisaidia kampuni ya Porsche kupiga hatua muhimu kuelekea kuungana na kampuni ya Volkswagen. Waziri mkuu wa jimbo la Baden Württemberg hapa Ujerumani, bwana Günther Öttinger, amesema kampuni ya Porsche itaweza kujisimamia na kujitangaza.

"Kampuni ya Porsche katika miaka 15 iliyopita imekuwa kampuni ya ufanisi mkubwa mashuhuri na yenye thamani kubwa katika uchumi wa Ujerumani. Katika siku za usoni, uasili wa kampuni ya Porsche sharti uonekane katika kampuni mpya itakayoundwa wakati itakapoungana na kampuni ya Volkswagen na nembo yake si swala la kujadiliwa."

Deutschland Streit um Hans Filbinger Ministerpräsident Günther Oettinger
Waziri mkuu wa jimbo la Baden-Wuerttemberg Guenther OettingerPicha: AP

Bwana Ötinger amemsifu mkuu wa kampuni ya Porsche aliyejiuzulu, Wendelin Wiedeking, kwa bidii yake ya kazi na alivyofaulu kuitoa kampuni hiyo kutoka katika hali ngumu ya kiuchumi na kuiongoza katika enzi ya ufanisi mkubwa na kuiwezesha kushindana na kupata faida kubwa katika kipindi cha miaka 16 ya uongozi wake.

Wiedeking, meneja anayepokea mshahara mkubwa Ujerumani nzima, na ambaye mkataba wake ulikuwa umalizike mwaka 2012, atapokea kitita cha Euro milioni 50 kama marupurupu ya mwisho. Nusu ya donge hilo nono atalitoa kwa ajili ya wakfu wa kijamii kuwasaidia wafanyakazi wa kampuni ya Porsche na wanahabari wazee wenye mahitaji.

Wafanyakazi wa Porsche wameridhika kwamba ufumbuzi umepatakina katika mzozo kati ya familia inayoimiliki kampuni hiyo na famili inayoimiliki kampuni ya Volkswagen. "Tunayo furaha kwamba hatimaye mzozo huu umemalizika kwa sababu ulikuwa unatughadhibisha. Sina mengi ya kusema. Kampuni ya Porsche inabakia kuwa Porsche na kampuni ya Volkswagen ni Volkswagen"

Bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Volkswagen itakutana mjini Stuttgart hapo kesho kujadili mustakabal wa kampuni ya Porsche.