Kiongozi wa Jamhuri ya Donetsk aapishwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kiongozi wa Jamhuri ya Donetsk aapishwa

Alexander Zakharchenko mwenye umri wa miaka 38 ameapishwa kuongoza kile kinachoitwa Jamhuri ya watu wa Donetsk baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi uliokosolewa na Ukraine na nchi za Magharibi

Alexander Zakharschenko kiongozi wa Jamhuri ya watu wa Donetsk

Alexander Zakharschenko kiongozi wa Jamhuri ya watu wa Donetsk

Alexander Zakharchenko mwenye umri wa miaka 38 ameapishwa kuongoza kile kinachoitwa Jamhuri ya watu wa Donetsk baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa kama zoezi la kumhalalisha hasa kwakuwa kulikuwa hakuna mpinzani aliyeshindana nae kwenye uchaguzi huo. Hata hivyo waasi wanasema kwamba uchaguzi huo umewapa fursa na uhalali wa kuyapigania malengo yao ya kujitenga.

Serikali ya Ukraine pamoja na nchi za Magharibi zinasema kwamba uchaguzi uliofanyika Jumapili unahatarisha kwa kiasi kikubwa makubaliano tete ya kusitisha vita ambayo yameshakiukwa kwa sehemu kubwa na ambayo yalifikiwa mwezi Septemba kwa kukuridhiwa kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa kote nchini humo lakini chini ya sheria za Ukraine.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akisisitiza juu ya kutoridhishwa kwake na hali iliyojitokeza na hasa kile alichokitaja kuhusika kwa Urusi katika mgogoro amesema bado hakuna sababu ya kuondowa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi.

Lakini amesisitiza kuwa na matumaini ya kupatikana suluhisho la kidiplomasia katika mgogoro huo wa Ukraine na kuongeza kwamba uchaguzi uliofanyika unaonyesha ni kwa jinsi gani kuna ugumu wa kuendeleza makubaliano yaliyofikiwa ikiwa uchaguzi huo usiohalali unakubalika.Urusi imeunga mkono uchaguzi huo mara baada ya kufanyika.Mapigano yalipungua baada ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita ingawa mashariki mwa nchi hiyo ya Ukraine bado yanashuhudiwa mapigano ya mara kwa mara.

Zakarchenko ameapishwa huku bendera ya jamhuri ya watu wa Donetsk ikipeperushwa na pia akila kiapo kwa kushikilia mkononi bibiblia hatua iliyochangia kupigiwa makofi na vifijo na umma uliohudhuria sherehe hiyo wengi wakiwa ni wapiganaji walikuwa wamebeba silaha.Ameahidi kuijenga upya Donetsk.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko akasirishwa na hatua ya Donetsk

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko akasirishwa na hatua ya Donetsk

''Nitabeba bango la watu wa Jamhuri ya Donesk kwa heshima.Tutayajenga makaazi yetu,mitambo yetu na migodi yetu tukiwa pamoja.Tutarudi katika makaaziy etu yaliyoharibiwa,tutawalea watoto wetu na kuwafunza kwa pamoja.Na hakuna mabomu au makombora yatakayofyetuliwa kwenye mitaa yetu.''

Katika sherehe hiyo wabunge kutoka Urusi na jimbo lililojitenga na Georgia la Abkhazia ambalo pia uhuru wake umetambuliwa na Urusi pekee na nchi nyingine tatu walihudhuria. Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameonya kwamba anafikiria kuondoa mashrti ya makubaliano ya kusitisha vita ya Septemba yaliyofikiwa pamoja na waasi wanaoiunga mkono Urusi- kutokana na uchaguzi huo alioutaja kuwa kitendo kisichokuwa halali.

Mwandishi Saumu Mwasimba

MharirI:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com