1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa IS Baghdadi auawa: Ripoti

Bruce Amani
27 Oktoba 2019

Kiongozi wa Kundi la Dola la Kiislamu - IS Abu Bakr al-Baghdadi inaaminika kuwa amekufa baada ya jeshi la Marekani kulishambulia eneo la Idlib nchini Syria

https://p.dw.com/p/3S111
Irak Abu Bakr al-Baghdadi
Picha: picture-alliance/AP Photo/Al-Furqan

Vyanzo vya habari vya Marekani vinaeleza kuwa, Baghdadi anaweza akawa ameuwawa kwa kujiripua wakati kikosi maalum cha Marekani kikiwa kinamlenga. Alikuwa akiwindwa na kikosi maalumu ambacho kilipewa idhini na Rais Donald Trump.

Kiongozi huyo wa Dola la Kiislamu ambae amekuwa akisakwa kwa muda mrefu na muungano wa kijeshi unaongozwa na Marekani dhidi ya IS, ameripotiwa kuuwawa kwa mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni. Baghdadi mwenye asili ya Iraq na umri wa miaka 48, aliunda mtandano madhubuti wa kile kinachoelezwa kuwa harakati za vita vya kidini na kuwa wapiganaji wenye nguvu, na mwaka 2014 kuanzisha mamlaka ya "ukhalifa" katika eneo kubwa la Syria na Iraq.

Wakati huo huo, Ikulu ya Marekani Jumamosi jioni imetangaza kwamba Rais Donald Trump atatoa taarifa nzito mapema leo hii, katika kipindi hiki kukikubikwa na taarifa ambazo hazijathibitishwa za operesheni za kijeshhi dhidi ya Kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria.

Naibu Msemaji wa Ikulu ya Marekani Hogan Gidley alitoa kauli hiyo pasipo kutoa ufafanuzi zaidi. Habari hiyo inafuatia ujumbe wa Twitter wa mapema jioni kutoka kwa rais Trump ambao ulisema "Jambo kumbwa limetokea hivi punde!" Hata hivyo wizara ya ulinzi ya Marekani imekataa kusema lolote kuhusiana na jambo hilo, pale shirika la habari la Ufaransa AFP lilipofanya mawasiliano nayo.