1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Boko Haram auwawa Nigeria

Admin.WagnerD25 Septemba 2014

Jeshi la Nigeria limedai kumuua kiongozi wa kundi la itikadi kali la Boko Haram, Abubakar Shekau, kama ikithibitika itakuwa hatua kubwa kwenye juhudi za jeshi hilo kulishinda kundi hilo la kigaidi la Nigeria

https://p.dw.com/p/1DKrE
Nigeria Boko Haram Abubakar Shekau Archiv
Abubakar Shekau, kiongozi wa kundi la Boko HaramPicha: picture alliance/AP Photo

Msemaji wa jeshi la Nigeria, Chris Olukolade, amewaambia waandishi wa habari mjini Abuja kwamba mpiganaji aliyekuwa na madevu mengi na aliyekuwa akijiita Mohammed Bashir ameuwawa wakati wa mapambano yaliyotokea kwenye mji wa Konduga kwenye jimbo la Borno. Kwa maneno mengine inasemekana kwamba Shekau alijibadili jina na kujiita Mohammed Bashir na ambapo pia alikuwa akionekana katika mikanda ya vidio ya Boko Haram akijitambulisha kama Abubakar Shekau, kiongozi wa Boko Haram

Kwa mara ya kwanza jeshi la nchi hiyo limetangaza hadharani kwamba Shekau ameuwawa baada ya huko nyuma kuweko madai ya duru za kiusalama kwamba aliuwawa Julai mwaka 2009 na mwishoni mwa mwaka 2013. Hata hivyo, katika tangazo lililotolewa jana na jeshi la Nigeria haikutajwa ameuwawa vipi na saa ngapi.

Utata wa kifo cha kiongozi wa Boko Haram

Mapema mwaka huu msemaji wa polisi ya upelelezi, Marilyn Ogar, alisema Shekau halisi alishauwawa na kwamba mtu anayejitokeza na kudai kwamba yeye ni Shekau kupitia mikanda ya video ya Boko Haram sio yeye bali ni kiini macho.

Abubakar Shekau Bekennervideo Boko Haram Nigeria 05.05.2014
Kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau akiwa katika operesheniPicha: picture alliance/AP Photo

Hata hivyo, jana msemaji wa jeshi la taifa, Olukalade, alisema utambulisho halisi wa kiongozi wa kundi hilo la Boko Haram haupo isipokuwa hilo jina Shekau limekuwa kama nembo kwa magaidi hao. Juu ya hilo akaongeza kusema kwamba jeshi la Nigeria litaendelea kutenda haki na kuchukua sheria kwa mtu yeyote atakayejipa cheo cha kuongoza kundi la Boko Haram pamoja na makundi mengine yanayotaka kukiuka uhuru na mamlaka ya taifa.

Ikiwa tangazo la kuuwawa Shekau litaumaliza utata na uvumi juu nchini Nigeria kuhusu ikiwa yu hai au amekufa ni suala la kusubiri na kuona. Ikumbukwe kwamba Shekau au Bashir alikuwa akijitambulisha pia kwa majina mengine kama Abacha Abdullahi Geidam na Damasak.

Upande mwingine akizungumza mbele ya kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Rais Goodluck Jonathan, aliutaka ulimwengu kuchukua hatua za haraka kukabiliana na kitisho kinachosababishwa na wapiganaji wa kundi hilo na mengine nchini mwake

Hayo yakitokea, mamia ya wanachama wa kundi la Boko Haram wanatajwa kwamba walijisalimisha hapo jana kwa mujibu wa msemaji wa jeshi. Kukamatwa kwa wapiganaji hao kumetokea baada ya mapambano makali kati ya jeshi na kundi hilo kaskazini mwa Nigeria na katika nchi jirani ya Cameroon.

Miongoni mwa hujuma zilizofanywa na kundi hilo hatari kabisa ni pamoja na kuwashikilia mateka wasichana wa shule zaidi ya 200 tangu mwezi Aprili na kwa miaka kadhaa limekuwa likiendesha kamepini ya kuwateka nyara watu, kuua, pamoja na kufanya mashambulizi ya kujitoa muhanga.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP/dpa/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef