Kiongozi wa upinzani Uganda atangaza kuondoka nchini
15 Machi 2026
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, ametangaza kuwa ameondoka nchini humo baada ya kujificha kwa karibu miezi miwili tangu kumalizika kwa uchaguzi wa rais uliofanyika Januari.
Katika video iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, amesema amelazimika kuikimbia Uganda kwa muda kwa sababu ya vitisho vya usalama baada ya uchaguzi huo. Hata hivyo hakufahamisha mahala alipo.
Uchaguzi wa Januari 15 ulimrejesha madarakani rais wa muda mrefu wa Uganda, Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, kwa muhula wa saba. Upinzani unasema matokeo ya uchaguzi huo yalijaa udanganyifu, madai ambayo serikali imekanusha.
Bobi Wine pia amesema akiwa nje ya nchi atafanya kampeni kimataifa ili kushinikiza vikwazo dhidi ya serikali ya Yoweri Museveni.
Ameongeza kuwa atarejea nchini siku zijazo, akisema kugombea urais si kosa la jinai.