1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinyanganiyiro cha Tiketi za mwisho za Kombe la dunia 2010

17 Novemba 2009

Leo Misri na Algeria: Ujerumani na Ivory Coast.

https://p.dw.com/p/KZGW
Logo Kombe la Dunia 2010

CHANGAMOTO LEO KOMBE LA DUNIA:

UGERUMANI NA IVORY COAST: MISRI NA ALGERIA:

Wakati Ujerumani, imemaliza msiba wa kifo cha kipa wake wa Taifa, Robert Enke na inarudi uwanjani jioni hii kujipima nguvu na mojawapo ya timu kali za Afrika katika Kombe lijalo la dunia-Tembo wa Ivory Coast, mjini Gelsenkirchen, bila ya nahodha Michael Ballack,macho ya mashabiki wa Afrika nzima, yanakodolewa Khartoum,Sudan kujua wapi na kwa mhanga gani ,tiketi ya mwisho ya kanda ya Afrika kucheza katika Kombe lijalo la dunia nchini Afrika Kusini itakwenda:Je, ni Misri au Algeria. Mashabiki na timu hizo mbili wameanza kuwasili Khartoum tangu Jumapili baada ya ule mpambano wa jazba na hamasa kubwa mjini Cairo . Ulinzi ni mkali umewekwa mjini Khartoum kuzuwia fujo na kumpunga shetani wa mpira.

Polisi wa Sudan, wamepiga timamu na wako tayari kuilinda usalama tangu jana mjini Khartoum huku mashabiki wa Misri na Algeria , wakiwasili kwa kile kila upande unachokiona "vita vya kufa-kupona" tangu kwa heshima ya dimba hata ya taifa.

Kwani, licha ombi la Misri kutolewa kwa serikali ya Algeria, ulinzi zaidi tangu kwa raia zake hata kwa mali zao,afisi za shirika la ndege la Misri-Egypt Air, mjini Algiers,zilihujumiwa na kuharibiwa tena na mashabiki wa Algeria, waliokasirika kwa kupigwa mawe basi la timu yao na kujeruiwa wachezaji wao 3.Ni chini ya kiini hicho, mpambano wa jioni ya leo unachezwa mjini Khartoum.

Gavana wa jiji la Khartoum Abderrahman al-Khidr,amewaambia maripota mjini Khartoum,vikosi vya usalama vimewekwa katika ulinzi wa hali ya juu.Akasema mashabiki 35,000 wataruhusiwa kuingia uwanjani unaosheheni kikawaida mashabiki 41,000 huko Omduramann , ili kuweza kuwatenganisha mashabiki wa timu hizo mbili.

Stadi wa Misri, Emad Motaeb, alietia lile bao la pili lililioiokoa Misri Jumamosi mjini Cairo, anatumai kutimiza ndoto nyengine ya kuwaongoza mafiraouni wenzake katika kombe la dunia 2010. Isitoshe, kocha wa Misri,mabingwa wa Afrika, wanaemuita sasa "Sultani" Hasan Shehata, anatumai Motaeb pamoja na Amr Zaki, watatamba leo mbele ya madume wa jangwani Algeria.

Kwahivyo, kinyan'ganyiro cha tiketi yamwisho leo ili Algeria au Misri, kujiunga na wenyeji Bafana Bafana,simba wa nyika-Kamerun,Black Stars-Ghana na Tembo wa Ivory Coast pamoja na Super Eagles Nigeria, ni vigumu kuagua kitamalizika vipi tangu kimatokeo hata kiusalama mitaani Khartoum;Cairo na Algeirs. Wamisri, wanatumai hatahivyo, kaburi waliowachimbia waalgeria Cairo,Jumamosi, watawafukia leo Khartoum.

Kuna mapambano mengine leo kanda ya ulaya kuamua hatima ya Ufaransa na Ireland huko Paris; Ureno bila ya Cristiano Ronaldo na Bosnia mjini Sarajevo.Ujerumani lakini, imeshakata sawa na Corte d'Ivire, tiketi yake ya kwenda 2010 Afrika kusini.Na jioni hii, bila ya nahodha wake Michael Ballack inapimana nguvu na mojawapo ya timu kali za Afrika-Ivory Coast ikiongozwa na nahodha Didir Drogba wa Chelsea.

Mpambano huu ,unachezwa chini ya wingu la huzuni ya kifo cha kipa wa Ujerumani, Robert Enke.Timu nzima ya Ujerumani, itavaa utambi mweusi mkononi na mchezo utasimamishwa kwa dakika 1 kumbumbuka marehemu kabla ya dimba kuanza uwanjani Gelsenkirchen,Ujerumani.

Ujerumani ,iliuvunja mpambano wa Jumamosi iliopita na Chile kutokana na msiba wa Robert Enke.Na leo asema kocha Joachim Löew , ni kuangalia usoni na kurejea kucheza dimba.

Mwandishi:Ramadhan Ali /AFPE/DPAE

Uhariri: Abdul-Rahma