1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KINSHASA: Bemba kwenda kwa matibabu Ureno

1 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDP

Ureno inasubiri idhini ya serikali ya jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumpokea kiongozi wa zamani wa waasi, Jean Pierre Bemba, anayethumiwa kwa makosa ya uhaini baada ya wafuasi wake kupapamba na majeshi ya serikali mwezi uliopita.

Makubaliano yamefikiwa kumruhusu Jean Pierre Bemba kwenda nchini Ureno kwa matibabu. Balozi wa Ureno nchini Kongo, Alfredo Duarte Costa, amesema makubaliano hayo yamefikiwa baina ya serikali ya mjini Kinshasa, tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUC, na Ureno.

Balozi Costa amesema Jean Pierre Bemba ameahidi kutojihusisha katika shughuli za kisiasa atakapokuwa mjini Lisbon, Ureno. Bemba atakuwa Ureno kwa wiki kadhaa kwa matibabu ya mguu wake ambayo wafuasi wake wanasema hayana uhusiano na machafuko ya hivi majuzi mjini Kinshasa.

Bemba ambaye alifanyiwa upasuaji mguuni mwezi Disemba mwaka jana katika hospitali moja mjini Lisbon, amekuwa katika ubalozi wa Afrika Kusini mjini Kinshasa tangu machafuko yalipozuka baina ya wafuasi wake na wanajeshi wa serikali mnamo tarehe 22 na 23 mwezi uliopita ambapo watu takriban 163 waliuwawa.

Mazungumzo ya kumuondoa Bemba nchini Kongo yamekuwa yakiendelea kwa siku kadhaa.