1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinga ya Corona bado safari ndefu

Lilian Mtono
5 Februari 2020

Shirika la afya duniani, WHO limepuuzilia mbali ripoti za vyombo vya habari hii leo kuhusiana na kile walichokitaja kama mafanikio ya uvumbuzi wa dawa za kuwatibu watu walioathirika na virusi vipya vya Corona.

https://p.dw.com/p/3XJls
China Impfungen in Shanghai
Picha: picture-alliance/dpa/W. Yadong

Ripoti iliyorushwa na kituo cha televisheni cha China imesema watafiti katika chuo kikuu cha Zhejiang wamegundua dawa yenye ufanisi mkubwa wa kutibu virusi hivyo vya Corona huku kituo cha televisheni cha Sky News cha Uingereza kikisema watafiti wamepiga hatua kubwa katika kutengeneza chanjo.

Msemaji wa WHO Tarik Jasaveric alipoulizwa kuhusu ripoti hizo alisema hakuna dawa yoyote inayojulikana kutibu kwa ufanisi virusi vya Corona. Mchakato wa kutengeneza na kufanya majaribio ya dawa ama chanjo dhidi ya aina yoyote mpya ya bakteria ama virusi huchukua muda mrefu na mara zote hukabiliwa na vizingiti. 

Ingawa utengezaji wa chanjo ya virusi vya Corona unafanywa kwa kasi kubwa hasa kutokana na ukuaji wa tekenolojia, lakini watafiti wanatarajia kuanza majaribio ya awali ya chanjo hiyo kwa binaadamu ifikapo Juni mwaka huu.

China: Angst vor weiteren Fällen des Coronavirus
Virusi vya Corna vimeendelea kusambaa na hali imezidi kuwa mbaya jijini WuhanPicha: Imago/W. Quanchao

Madaktari wanaoangazia namna ya kuwatibu waathirika wa Corona huenda wakajaribu dawa za kujikinga na virusi zilizopewa leseni ya kutumika dhidi ya maambukizi mengine ya virusi ili kuona kama zinaweza kusaidia lakini katika wakati ambapo dawa muhimu za kujikinga na virusi ikiendelea kutengenezwa.

Hali katika mji wa Wuhan ambako ni kitovu cha virusi hivyo bado ni mbaya hii ikiwa ni kulingana na maafisa wa jiji hilo. Watu wameendelea kutengwa kwenye vyumba vya hoteli, shule na hospitali binafsi.

Mkuu wa benki kuu ya Ulaya, Christine Lagarde amesema kusambaa kwa virusi vya Corona nchini China na kwingineko duniani kunaibua sintofahamu mpya kwa uchumi wa Ulaya.

Lagarde amesema kwenye hotuba yake mjini Paris na kuongeza kuwa wakati kitisho cha vita vya kibiashara kati ya Marekani na China kikionekana kupungua, virusi vya Corona vinaibua safu mpya ya sintofahamu.

Taarifa ya habari, saa 12:00 asubuhi (Afrika Mashariki)

Matamshi ya Lagarde yanafuatia taarifa ya mwenyekiti wa benki kuu ya Marekani Jerome Powell wiki iliyopita kwamba benki hiyo ilikuwa inafuatilia kwa karibu mripuko wa virusi hivyo ambao umekwishasababisha vifo vya takribani watu 500 huku zaidi ya 24,000 wakiwa wameambukizwa katika eneo la China Bara kusambaa kwenye mataifa zaidi ya 20. Kiasi raia wa Marekani 350 wamekwishaondolewa Wuhan.

Huko Indonesia maelfu ya watalii wamekwama mjini Bali baada ya serikali kuahirisha safari za ndege kutoka na kwenda China Bara, kufuatia wasiwasi wa virusi hivyo. Takribani watalii 5,000 hivi sasa wapo mapumzikoni kwenye kisiwa hicho. Kaimu gavana wa Bali Tjokorda Oka Artha Ardhana Sukawati amesema wanaweza kuwaongezea muda wa vibali vya kuwepo nchini humo baadhi ya watalii.

DW imefanya mahojiano na mwanafunzi raia wa Nigeria aliyeko Wuhan kwa miaka minne sasa. Mwanafunzi huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Halima amesema tangu kutokea kwa mripuko huo maisha yamekuwa magumu sana. Amesema wamefungiwa ndani kwa zaidi ya siku nane na kila mmoja anaogopa kutoka nje.