1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nahodha wa Ujerumani asema wachezaji wanafanya mazungumzo.

Shisia Wasilwa
20 Juni 2018

Nahodha wa timu ya Ujerumani amesema, kuwa wachezaji wa timu hiyo ya kandanda wamekuwa wakifanya mazungumzo baina yao. Timu hiyo lazima icheze vizuri lakini kitu kinachotia moyo ni kuwa wachezaji wanalifahamu hilo vyema.

https://p.dw.com/p/2zwde
Fußball WM 2018 Gruppe F Deutschland - Mexiko
Picha: Reuters/M. Shemetov

Kwenye mechi yake ya ufunguzi dhidi ya Mexico Manuel Neuer ambaye ndiye nahodha alichelewa kufika kwenye kikao na wanahabari kwa yumkini nusu saa. Sababu ya kuchelewa kwake kufika inaacha kwa upande mmoja  maswali mengi kuliko majibu.

"Samahani. Tulikuwa na mkutano wa timu nzima uliochukua muda mrefu zaidi ya ilivyotarajiwa, "Neuer alisema. "Sisi wenyewe ni wakosoaji wakuu wa mchezo wetu na tumevunjika moyo na kukasirishwa jinsi tulivyocheza dhidi ya Mexico.

Tangu kushindwa kutamba, yaelekea kuwa Ujerumani imebadilisha mahusiano yake na wanahabari. Mkutano na waandishi habari uliokuwa umeratibiwa kufanyika Jumatatu na Phillip Lahm nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani ulifutiliwa mbali huku mazoezi ya kikosi hicho yakifanyika kwa siri kwa lengo la kufanya vyema zaidi kwenye mchezo wao utakaofuatia. Hata muda wa mkutano na waandishi habari umepunguzwa hadi dakika 15 tu, ambao pia ni vigumu kufanyika.

Nahodha wa Ujerumani Manuel Neuer
Nahodha wa Ujerumani Manuel Neuer Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

"Hakuna anayekataa kuwajibika. Tulizungumza kuhusu huo mchezo kwenye basi na pia tunazumgumza wakati wote wa maakuli." Anasema Neuer bila ya kuficha.

Maswali mengi yameulizwa kuhusu kikosi hiki cha Ujerumani kabla na baada ya michuano ya dimba la Kombe la Dunia kuanza na kushindwa kwao na Mexico. Sasa wachezaji wenyewe wanajiuliza maswali.

"Tulikosa ujasiri, imani na maelewano. Kwanini, sijui," anafichua Neuer kwenye mkutano na waandishi habari. "Hatukuwa tayari wakati wa mchuano huo. Sababu kubwa ilikuwa viongozi kwenye kikosi. Hatukuweza kujipanga na kuudhibiti mchezo uwanjani."

Wakati wa viongozi kuchukua usukani

Pengine wakati huu tunawakosa wachezaji kama vile Per Mertesacker ama Bastian Schweinsteiger, lakini kikosi hiki kina viongozi. Wanahitaji tu kuchukua usukani.

Kikosi cha Ujerumani baada ya kushindwa na Mexico
Kikosi cha Ujerumani baada ya kushindwa na MexicoPicha: Getty Images/M. Hangst

Ni bora kuongeza kuwa kutetea taji la Kombe la Dunia ni vigumu kuliko kulitafuta. Pengine Ujerumani imepuuzilia hilo. Katika miezi michache iliyopita hawajakuwa wakitafutia ufumbuzi matatizo yanayowazonga. Kikosi hiki hakiwezi tena kuchukua  hatua za kupuuza.

Ujerumani sasa inahitaji kuimarisha kikosi chake kabla ya mechi yake ijayo dhidi ya Sweden siku ya Jumamosi.

"Tumeboresha mazungumzo kati yetu zaidi ya ilivyokuwa kabla ya kushindwa na Mexico, anasema Neuer. "Wachezaji wengi wanahusika. Tunaamini tutafika kwenye awamu ya mtoano."

Sio vigumu kuamini anavyosema Neuer, hasa kwa sababu nahodha huyo huenda alizembea kutokana na taarifa zilizokuwa zikienea kuhusu timu ambazo hucheza dhidi ya Ujerumani. Badala yake alielezea kwa kina hali ya mambo yalivyo katika kikosi hicho.

"Kipindi cha kwanza kwenye mchezo kati yetu na Mexico tulitanabahishwa. Hatuhitaji kipindi kingine kama hicho." Neuer alisema. Iwapo Ujerumani inahitaji kutanabahishwa tena, watajilaumu wenyewe."

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Jonathan Harding

Mhariri: Yusuf, Saumu