1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim kwa Trump: Heri ya Mwaka Mpya, lakini usitujaribu!

Daniel Gakuba
1 Januari 2019

Katika hotuba yake ya mwaka mpya kwa taifa lake, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameionya Marekani dhidi ya kusisitiza hatua za upande mmoja, vinginevyo, watatafuta njia nyingine.

https://p.dw.com/p/3AqGC
Nordkorea  | Neujahrsansprache Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, akitoa hotuba ya Mwaka MpyaPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/KRT

Kim Jong Un amesema anataka kuendeleza mazungumzo na Marekani kuhusu kuondoa silaha za nyuklia kwenye Ras ya Korea, lakini akatoa tahadhari, akisema hawataki uwezo wao wa kuwa na subira uwekwe majaribuni.

Kiongozi huyo wa kiimla amesema katika hotuba yake, kwamba anataka mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini yasifanyike tena, na Marekani iache kuweka silaha za kivita nchini Korea Kusini.

Ameonya juu ya uwezekano wa nchi yake kutafuta njia nyingine, ikiwa Marekani 'itaendelea kuvunja ahadi ilizozitoa, na kubeza subira ya watu wa Korea Kaskazini, kwa kuwataka wachukue hatua kadhaa wakati ikiendeleza vikwazo na shinikizo' dhidi ya nchi yao.

''Ikiwa Marekani haitatimiza ahadi ilizozitoa mbele ya macho ya ulimwengu mzima,'' amesema Kim, ''tunaweza kukosa chaguo jingine mbali na kufuata njia mpya katika kulinda uhuru wetu na kutetea maslahi yetu.''

Marekani yatakiwa kurejea kwenye meza ya mazungumzo

Kim Jong Un amesema Korea ya Kaskazini imekwishaonyesha utashi wa kuchukua hatua katika kuondoa silaha za nyuklia, lakini Marekani inapata kuridhia mengi zaidi.

''Ikiwa Marekani itafanya juhudi za dhati na hatua zinazokwenda sambamba na matendo yetu ya mfano, basi uhusiano baina yetu utaboreka kwa kasi, kupitia mchakato wa kutekeleza hatua hizo za awali.'' Alisema Kim, akiwa amekaa katika kiti kilichotengenezwa kwa ngozi.

''Ni msimamo usiotetereka wa chama chetu na Jamhuri yeti, na ni dhamira yangu thabiti kwamba kama ilivyotangazwa baada ya mkutano wa Juni 12...kuchukua hatua za kuweka amani ya kudumu na kuondoa kikamilifu silaha za nyuklia kutoka kwenye Ras ya Korea.'' Aliongeza.

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini amehimiza uhusiano imara kati ya Korea mbili, akisisitiza kuwa upande wake uko tayari kuanzisha tena shughuli za pamoja za viwanda kwenye eneo la mpakani la Kaesong, na kuanzisha tena safari za Wakorea Kusini kutembelea ''Milima ya Almasi.'' Lakini, ili haya yote yawezekane, shart´i Korea Kaskazini iondolewe vikwazo.

Hotuba ya Mwaka Mpya ni tukio muhimu kwenye kalenda ya kisiasa ya Korea Kaskazini, kwa sababu inaweka agenda ya mipango ya mwaka unaofuata.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,rtre,ape,dpae

Mhariri: Sekione Kitojo