1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi cha Olimpiki Kenya kupiga kambi Eldoret

29 Aprili 2016

Maafisa wa Chama cha Riadha ya Kenya wameuchagua mji wa Eldoret kuandaa majaribio ya wanariadha watakaofuzu katika Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro mwezi Agosti

https://p.dw.com/p/1IfSk
China Beijing 2015 IAAF Weltmeisterschaft Nicholas Bett
Picha: picture-alliance/dpa/F. Robichon

Itakuwa mara ya kwanza ambapo kikosi cha Kenya kitachaguliwa katika majaribio yatakayofanywa nje ya mji mkuu Nairobi, ambao umekuwa ukitumiwa katika shughuli hiyo kwa ajili ya mashindano ya Olimpiki na ya ubingwa wa dunia. Maafisa wa riadha wanasema wameuchagua mji wa Eldoret kwa sababu wanariadha wengi wanaotaka kushiriki katika Olimpiki wanafanya mazoezi yao na wanatoka katika eneo hilo.

Majaribio ya kikosi cha Kenya yataandaliwa kati ya Juni 14 na 16. Kikosi hicho kitapiga kambi katika eneo hilo kabla ya kuelekea Brazil.

Na mmoja wa wanaotarajiwa kuchaguliwa katika kikosi cha Kenya ni bingwa wa mbio za mita 400 kuruka viunzi Nicholas Bett, ambaye aliushangaza ulimwengu kwa kushinda taji la ulimwengu katika mashindano ya riadha ya dunia mjini Beijing 2015. Bett anasema safari yake haijawa rahisi sana maana ameruka viunzi vingi maishani kabla ya kupata mafanikio ya kuruka viunzi vya uwanjani….na anamshukuru babake ambaye alimpa motisha wakati akiwa angali mtoto

Bett anasema ratiba yake ya mashindano ya mwaka huu ni ngumu kuliko ya mwaka jana, lakini atafanya juu chini kuhakikisha kuwa anajiandaa vya kutosha

Brazil kwa muda mrefu inafahamika kuwa nchi ambayo inaweza kuandaa tafrija kubwa na tayari maandalizi ya Michezo ya Olimpiki yanakamilika. Sasa ni wakati wa kuwalaki wageni.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Iddi Sessanga