1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi cha NATO chaomba msamaha

Thelma Mwadzaya16 Aprili 2009

Wanajeshi wanaosimamiwa na kikosi cha NATO nchini Afghanistan wamekiri kuwaua raia 6 wa nchi hiyo katika shambulizi la angani jimboni Kunar.

https://p.dw.com/p/HYWV
Majeshi ya Marekani yaliyoko KabulPicha: AP
Hamid Karzai PK in Kabul
Rais wa Afghanistan Hamid KarzaiPicha: AP

Vifo vya raia vinavyosababishwa na operesheni za wanajeshi wa kigeni wanaowasaka wapiganaji wa Taleban vimesababisha mvutano kati ya serikali ya Afghanistan na mataifa ya magharibi yanayosimamia operesheni hizo.Kufuatia hali hiyo Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amemtaka kiongozi wa kikosi cha NATO kufafanua makosa hayo


Kwa mujibu wa taarifa ya kikosi kinachosimamiwa na NATO nchini Afghanistan uchunguzi wa pamoja umebaini kuwa raia sita na wanamgambo wanne wameuawa baada ya shambulio la angani la Jumatatu.Uchunguzi huo umeishirikisha serikali ya Afghanistan na kikosi hicho cha NATO.Raia wengine 14 walijeruhiwa.Wanajeshi wa Marekani kwa upande wao walikiri kuwauwa raia watano wiki iliyopita katika jimbo la Khost.


Hii leo Rais wa Afghanistan Hamid Karzai alimtaka kamanda wa kikosi cha mataifa ya magharibi nchini humo Jenerali David McKiernan wa Marekani kufafanua taarifa hiyo.

Jenerali McKiernan kwa upande alimhakikishia Rais Karzai kuwa watashirikiana na wanajeshi wa Afghanistan ili kuepukana na visa hivyo.Kiongozi huyo wa kijeshi pia alisikitishwa na hali hiyo japo majeshi ya NATO kwa pamoja na yale ya muungano yanajitahidi kutowalenga raia wa kawaida.Kamanda huyo aliongeza kuwa ujumbe huo utazisaidia familia zilizofiliwa.


Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya kikosi hicho shambulio la Jumatatu liliwalenga wapiganaji wanaoendesha operesheni zao katika eneo ambalo kwa kawaida halina wakazi ambao ni raia wa kawaida.

Kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu na seriakli ya Afghanistan idadi ya vifo vya raia vinavyosababishwa na operesheni za wanajeshi wa kigeni wanaowasaka wapiganaji wa Taleban inaripotiwa kuongezeka tangu mwaka mmoja uliopita. Hivi karibuni makamanda wa vikosi hivyo wamethibitisha kuwa vitendo hivyo vimewafanya raia wa Afghanistan kutokuwa na imani nao.Makamanda hao wamesisitiza kuwa kwa sasa wanachukua hatua za ziada zinazoazimia kupunguza vifo vya raia wa kawaida,kufanya uchunguzi wa vitendo hivyo kadhalika kuomba msamaha punde mauaji yanapotokea.

Wakati huohuo mwanajeshi mmoja wa kikosi cha ISAF aliuawa hapo jana baada ya bomu la kutegwa barabarani kulipuka kwenye eneo la mashariki mwa Afghanistan.Wengi ya wanajeshi wa Marekani wanashika doria katika eneo hilo.Marekani inapanga kupeleka wanajeshi na washauri wa masuala ya kijeshi wa ziada wapatao alfu 21 nchini Afghanistan kabla uchaguzi wa rais kufanyika nchini humo

Kwa upande mwengine Uholanzi inaandaa mkutano maalum wa mawaziri wa Ulinzi kutoka mataifa 8 yanayochangia katika ujumbe wa NATO wa Afghanistan.Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Uholanzi kikao hicho kinachofanyika kila baada ya miezi sita kimepangwa kufanyika ifikapo tarehe 10 na 11 mwezi wa Juni katika mji wa Houthem Sint Gerlach unaopakana na Ujerumani na Ubelgiji.

Mkutano huo utawaleta pamoja mawaziri wa Ulinzi kutoka mataifa ya Australia,Canada,Denmark,Estonia,Romania,Uingereza,Marekani na mwenyeji Uholanzi.

Yapata wanajeshi alfu 2 wa Uholanzi wanashika doria nchini Afghanistan hususan katika eneo la kusini la Uruzgan chini ya mwamvuli wa kikosi kinachoongozwa na NATO cha ISAF.

Jumla ya wanajeshi alfu 70 wa kigeni wanajitahidi kupambana na wanamgambo wanaoipinga serikali iliyoingia madarakani baada ya kungolewa kwa utawala wa Taleban mwaka 2001.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa zaidi ya raia alfu 2 wa Afghanistan waliuawa mwaka uliopita katia mazingira kama hayo.


Mwandishi:Thelma Mwadzaya/ RTRE/AFPE

Mhariri:M.Abdul-Rahman