1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiir ataka maridhiano na kusameheana

17 Januari 2011

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amewaomba watu wa eneo hilo kuwasamehe Waislamu wa Sudan Kaskazini kutokana na vita vilivyokuwapo, huku matokeo kidogo ya kura ya maoni yakionyesha uwezekano mkubwa wa eneo hilo kujitenga.

https://p.dw.com/p/zycM
Kijana wa Sudan ya Kusini akibeba bendera ya eneo hilo
Kijana wa Sudan ya Kusini akibeba bendera ya eneo hiloPicha: picture alliance/dpa

Katika matamshi ya kwanza aliyotoa tangu kumalizika kura ya maoni katika eneo la Kusini lililo na idadi kubwa ya waumini wa Kikristo, Rais Salva Kiir alijiunga na maelfu ya waumini katika kushukuru kufanyika kura hiyo na kuliombea litakalo kuwa taifa lao wakati wakisubiri matokeo rasmi.

Waandalizi wanaendelea na shughuli za kuhesabu kura hii leo, zitakazoamua hatima ya uhuru wa Sudan Kusini baada ya sehemu ya matokeo kutoka vituo vya upigaji kura kuonyesha uwezekano mkubwa wa kujitenga eneo hilo. Ujumbe wa waangalizi wakuu wa nje, Umoja wa Ulaya na Taasisi ya Carter ya aliyekuwa rais wa Marekani Jimmy Carter, walitarajiwa kutoa ukaguzi wao wa jinsi kura hiyo ya wiki nzima ilivyokuwa.

Matumaini ya Mwanzo Mpya

Awali, seneta wa Marekani John Kerry ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya uhusiano wa nchi za nje alisema kura hiyo hiyo ya maoni inaashiria enzi mpya kwa Sudan ya Kusini na Kaskazini pia.

Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, ambaye taasisi yake inashiriki kwenye uangalizi wa kura ya maoni ya Sudan ya Kusini
Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, ambaye taasisi yake inashiriki kwenye uangalizi wa kura ya maoni ya Sudan ya KusiniPicha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama amesema katika taarifa yake kuwa waangalizi hao walitiwa moyo na uaminifu uliokuwepo katika shughuli nzima mpaka leo, na kuongeza kuwa idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura, iliutia moyo ulimwengu. Rais Obama aliongeza kuwa kura hiyo ilidhihirisha jitihada za watu na viongozi wa Sudan Kusini kuunda mustakabali mwema.

Vituo vya upigaji kura katika eneo hilo vilitarajiwa kumaliza kuhesabu kura hizo, hii leo.

Katika mji mkuu wa Juba vituo vya kwanza vya kura vilvyowasilisha matokeo ya kura zilizopigwa,vilidhihirisha wingi wa kura za kuunga mkono kujitenga kwa eneo hilo kutoka kwa Sudan kaskazini na kuufungua ukurasa mpya baada ya miongo mitano ya mzozo ulioliathiri taifa lililokubwa barani Afrika.

Matokeo ya Awali

Katika kituo kilichowekwa karibu na kumbukumbu za kiongozi muasi, John Garang aliyetia saini mkataba wa mwaka 2005 uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe, muda mfupi kabla ya kufariki, matokeo ya kituo D yalikuwa ni kura 3,066 za kuunga mkono kujitenga huku 25 pekee zikiunga mkono Kusini kuungana na kaskazini.

Wafuasi wa Salva Kiir wakifurahia tangazo la kura ya maoni ya Sudan ya Kusini
Wafuasi wa Salva Kiir wakifurahia tangazo la kura ya maoni ya Sudan ya KusiniPicha: picture-alliance/dpa

Jopo la Umoja wa mataifa lililoundwa kuangalia kura hiyo lilionya kuwa licha ya kuwa Wasudani wangependa kujuwa matokeo ya kura hiyo kwa haraka, wanawaomba wasudani kuwa na subira na kutambua kuwa matokeo yatakayo tolewa na maafisa wa kura hiyo ya moani pekee ndiyo yalio rasmi.

Matokeo ya mwisho kubaini iwapo eneo hilo linajitenga na kuwa nchi mpya duniani mwezi Julai, hayatarajiwi kutolewa kabla ya mwezi ujao.

Umoja huo wa Mataifa pia umesisitiza umuhimu wa kulindwa raia katika wiki zinazokuja baada ya kutokea uvamizi dhidi ya Wasudani kusini waliokuwa wakirudi kutoka kaskazini kwa ajili ya kura hiyo ya maoni, na kusababisha vifo vya watu 10.

Mzozo wa Abyei

Waziri wa mambo ya ndani wa Sudan Kusini, Gier Chuang anatarajiwa kusafiri hii leo kuelekea katika mji wa Kaskazini , Kadugli, kwa mazungumzo na waziri wa mambo ya ndani Ibrahim Mohammed Ibrahim, na viongozi wanaozozana wa eneo la Abyei wa makabila ya Ngok Dinka, na waarabu wa Misseriya, yanaonuiwa kumaliza vurugu.

Mratibu wa misaada wa Umoja wa mataifa nchini Sudan, Georg Charpentier, amesema mazungumzo hayo yalioandaliwa na Umoja huo wa mataifa, yananuiwa kuendeleza mkutano wa awali kati ya viongozi wa makabila hayo mawili, uliolainisha hali wiki iliyopita.

Mwandishi: Maryam Abdalla/AFPE

Mpitiaji: Hamidou Oummilkheir