Kigeugeu cha Yahya Jammeh na Misaada ya Maendeleo kwa Afrika | Magazetini | DW | 16.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Kigeugeu cha Yahya Jammeh na Misaada ya Maendeleo kwa Afrika

Muimla hakubali kushindwa, homa ya Malaria, na Mkakati mpya wa misaada kwa Afrika ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

 

Tunaanzia lakini Gambia ambako kigeugeu cha rais Yahya Jammeh kimegonga vichwa vya habari vya magazeti takriban yote ya humu nchini. Kwanza baada ya Jammeh kuwashangaza walimwengu alipokubali kushindwa katika uchaguzi wa rais na kumpongeza mpinzani wake Adama Barrow wa muungano wa upande wa upinzani na baadae aliposema hakubaliani na aliyoyasema, na kuhimiza uchaguzi uitishwe tena."Muimla haregezi kamba" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Süddeutsche" linalochambua kigeugeu hicho cha Yahya Jammeh. Anang'ang'ania madaraka", linaendelea kuandika gazeti hilo la mjini Münich linalokumbusha yale aliyowahi kuyasema kiongozi huyo aliyeitwala Gambia kwa zaidi ya miaka 20, "atakuwa tayari kuitawala nchi hiyo kwa miaka bilioni moja, Mungu akipenda."

Süddeutsche Zeitung limekumbusha alichokisema Jammeh kwamba asingeendelea kutawala kinyume na matakwa ya wananchi. Maneno matupu na ahadi za uongo linaendelea kuandika gazeti hilo la mjini Munich linalohisi hatima ya nchi hiyo itategemea msimamo wa jeshi. Hakuna ishara nzuri linamaliza kuandika Süddeutsche Zeitung, baada ya kumnukuu kiongozi wa vikosi vya wanajeshi jenerali Ousmane Badjie akisema "analipwa na serikali ya Yahya Jammeh, anapokea amri kutoka kwake tu na kwamba jukumu lake ni kuhakikisha usalama na amani nchini."

 Kitisho cha Machafuko Gambia

Maoni sawa na hayo yameandikwa na mhariri wa gazeti la mjini Berlin die Tageszeitung. Gazeti linazungumzia juhudi za upatanishi za jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika Magharibi Ecowas na wito wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kumtaja Jammeh ang'atuke."Yote hayo hayamshughulishi,linaandika die Tageszeitung linalomnukuu mwenyekiti wa muungano wa upande wa upinzani Fatoumata-Jallow-Tambajang akitoa wito Jammeh akamatwe."Haaminiki,kila anapovumiliwa ndipo hatari ya kusababisha machafuko inapozidi kuwa kubwa, amenukuliwa Fatoumata Jallow Tambajang akisema.

Lengo la kupunguzwa hadi nusu idadi ya wanaokufa kwa Malaria liko mbali kufikiwa

Frankfurter Allgemeine linamulika juhudi za kupambana na homa ya Malaria barani Afrika ambako gazeti hilo linasema maradhi hayo yanayoziathiri nchi za joto yanasababisha watu laki nne kufa kwa mwaka barani Afrika na  mtoto mmoja kufariki kila dakika mbili . Frankfurter Allgemeine limechapisha ripoti ya mwaka huu ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO inayodhihirisha kwamba idadi ya wanaoambukizwa imepungua kwa asili mia 21 katika kipindi cha miaka 5 iliyopita , na kwamba nchi sita zimefanikiwa kuyashinda nguvu maradhi hayo-nchi nyengine 11 hazijashuhudia kadhia mpya za walioambukizwa tangu angalao miaka mitatu iliyopita, hata hivyo Frankfurter Allgemeine linasema lengo lililowekwa la kupunguzwa kwa hadi asili mia 40 idadi ya  kadhia za homa ya malaria na idadi ya vifo vinavyosababishwa na homa hiyo, halitaweza kufikiwa hadi ifikapo mwaka 2020.

Mkakati wa aina mpya wa kulisaidia bara la Afrika

Lilikuwa gazeti la masuala ya kiuchumi Handelsblatt la mjini Düsseldorff lililozungumzia kuhusu mkakati wa aina mpya wa kulisaidia bara la Afrika. Mkakati uliokuwa ukitumika hadi sasa katika kutoa misaada ya maendeleo haujasaidia kitu, waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Gerd Müller anabuni mkakati wa aina mpya unaolingana na ule wa Marshallplan. Mkakati huo unalenga kuzuwia wimbi la wakimbizi wanaokuja Ulaya kwa kubuni nafasi zaidi za kali na kuimarisha uchumi katika nchi za Afrika.

Kwa upande wake Frankfurter Allgemeine linapinga fikra ya kubuniwa mpango wa kutolewa misaada kama ule uliotumika baada ya vita vikuu vya pili vya dunia au Marshall Plan kama unavyojulikana. Gazeti linasema fedha nyingi kutoka nchi tajiri za kaskazini ndizo zinazozifanya nchi za Afrika kuzidi kuwa maskini. Gatezi hilo limeutaja uamuzi wa kundi la wataalam, wanadiplomasia na wengineo walikutana mjini Cologne kuzungumzia namna ya kulisaiadia bara la Afrika.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ BASIS/PRESSEM/ALL/PRESSE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo