1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha Ted Kennedy

Oumilkher Hamidou27 Agosti 2009

Huzuni za walimwengu kwa kifo cha mwanasiasa mashuhuri kabisa wa Marekani

https://p.dw.com/p/JJJj
Senetor Edward Kennedy na rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

Kifo cha senetor Edward Kennedy,kisa cha kualikwa mkuu wa benki ya Ujerumani Deutsche Bank kusherehekea siku yake ya kuzaliwa katika ofisi ya kansela mjini Berlin na dalili za kuchipuka upya shughuili za kiuchumi nchini ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanzie Marekani lakini ambako kifo cha senetor Edward Kennedy,kitindamimba katika familia mashuhuri katika siasa ya Marekani,kimeihuzunisha dunia nzima.

Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika:

Ted Kennedy ameileta pamoja familia na kisiasa alifanikiwa kushawishi hali ya mambo kuliko mwanasiasas yeyote mwengine wa chama cha Democrats.Obama ana mengi ya kumshukuria.Hata hivyo kivuli cha nduguze,Kennedy amekwenda nacho kiyama.Hatas hivyo hakuna anaeweza kufananisha kifo chake na kile cha nguduye John watu wakikumbuka alikuwa wapi aliposikia juu ya kuuliwa kwake huko Dallas.

Gazeti la Braunschweiger Zeitung linaandika:

Edward Kennedy ameliwakilisha jimbo la Massachussets kwa muda wa miaka 46 katika baraza la Senet.Hakua tuu mwakilishi wa chama cha Democratics,alikua taasisi hasa.Alipania kuilinda demokrasia nchini Marekani. Ukakamavu wake ndio uliomfanya Edward Kennedy, aendelee kuamini malengo ya dola huru ambako kila mtu ana nafasi ya kujiimarisha.Kennedy ni mwanasiasa ambae juhudi zake zinastahiki kuvuliwa kofia."

Josef Ackermann bei Angela Merkel im Kanzleramt
Kansela Angela Merkel na mkuu wa Deutsche Bank Josef Ackermann ,msimu wa kiangazi mwaka janaPicha: picture-alliance/dpa

Mada yetu ya pili inahusiana na kisa cha kualikwa mwenyekiti wa benki mashuhuri ya Ujerumani Deutsche Bank Josef Ackermann kusherehekea siku yake ya kuzaliwa katika ofisi ya kansela mjini Berlin.Wahariri wanakubaliana mada hiyo imekuzwa tuu kwasababu za kampeni za uchaguzi.Gazeti la "Sächsische Zeitung" linaandika

Ingekua kashfa kama kansela Merkel alimualika mkuu wa Deutsche Bank Josef Ackermann na kundi la wacheza tufe kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.Ukweli lakini ni kwamba mkuu huyo wa benki alitaka kujifakharisha alipojinata kupitia kituo cha televisheni eti kansela amemshauri asherehekee siku yake ya kuzaliwa katika makao makuu ya serikali na awaalike marafiki zake 30.Mwaliko kweli umetokana na kansela,lakini aliyeupigia upatu ni Josef Ackermann.La kusemwa hapa ni kwamba kansela ana haki ya kumualika amtakae.

Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung linahoji Kansela Merkel sio wa mwanzo .Gazeti linaendelea kuandika:

Bila ya shaka kiongozi wa serikali anaruhusiwa kumualika mtu yeyote anaehisi wadhifa wake ni muhimu na wa maana.Hata Gerhard Schröder ambae kimsingi si shabiki wa aliyeshika nafasi yake ,amesema hivyo hivyo.Mwaliko kama huo wa kundi dogo unasaidia kubadilishana maoni na kuondowa dhana na pengine hata kuepusha makosa yasitokee siku za mbele.Faida kama hiyo ni kubwa mtu hawezi kuilinganisha na yuro wala senti.

Mwandishi:O.Hamidou/Dt Zeitungen

Mhariri:M.Abdul-Rahman