Kifo cha Magufuli chatawala magazeti ya Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magufuli awashughulisha wahariri wa Ujerumani

Kifo cha Magufuli chatawala magazeti ya Ujerumani

Kifo cha Magufuli chatawala magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yamegusia masuala mbali mbali ya barani Afrika na mojawapo ni kifo cha rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ,na hali ya kutisha katika jimbo la Tigray huko nchini Ethiopia.

Die Zeit

Mhariri wa gazeti hilo ameanza kwa kichwa cha maneno kinachosema rais wa Tanzania afariki dunia. kilichomuua ni ugonjwa wa moyo.Mhariri huyo anaendelea kusema kwamba ulikuweko uvumi juu ya afya ya kiongozi huyo kwa siku kadhaa na sasa rais Magufuli amefariki. Sababu ya kifo chake kilichotokea jumatano yaumkini ni tafauti kabisa na kile watu walichokishuku,Magufuli hakufariki kwa Covid-19 bali kwa ugonjwa wa moyo kama alivyotangaza makamu wa rais Samia Suluhu ambaye sasa ni rais wa nchi hiyo. Rais John pombe Magufuli awali alitoweka machoni mwa hadhara ya Tanzania kwa kipindi kirefu na kusababisha kuibuka tetesi nyingi kuhusu ugonjwa wa Covid-19. Mhariri huyu wa gazeti la Die Zeit anakwenda mbali zaidi na kusema Magufuli kwa muda mrefu alipuuza hatari ya virusi vya Corona katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kusababisha ukosoaji duniani kwa kuibuka kauli za kichokozi na kejeli. Kwa malezo ya mhariri huyu wa Die Zeit,Magufuli aliyeingia madarakani mwaka 2015 aliikwamisha Tanzania nchi ya wakaazi takriban milioni 58.Kiongozi huyo aliyepewa jina Bulldozer aliikwamisha Tanzani kwasababu ya uongozi wake wa kutowasikiliza wengine,ambaye waliomuunga mkono walimuona kama kiongozi aliyesukuma mbele maendeleo ya nchi kwa ujenzi miradi mikubwa ya miondo mbinu na kutetea maslahi ya Tanzania kwa kujiamini. Mhariri wa gazeti hilo anamalizia kwa kuandika Hata hivyo hali ya haki za binadamu chini ya Magufuli ilidorora kwa kiwango kibwa. Wakosoaji na watetezi wahaki za binadamu walilaani hatua zake za kuzuia uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza pamoja na harakati za vyama vya upinzani.

Gazeti la Franfurter Allgemeine la mjini Frankfurt nalo pia limeandika juu ya kifo cha rais wa Tanzania John Pombe Magufuli na mhariri wa gazeti hilo yeye anaanza kwa kusema kwamba katika mitandao ya kijamii hisia za watu wengi zinaonyesha kwamba,wanataraji sasa Tanzania itabadili mkondo katika mapambano dhidi ya janga la virusi vya Corona baada ya kifo cha rais Magufuli. Mhariri wa gazeti hilo anasema Magufuli alikuwa kiongozi mbishi sana barani Afrika aliyelipuuza kabisa janga la virusi vya Corona. Sasa amefariki akiwa na umei wa miaka 61 na kwa mujibu wa taarifa za serikali amefariki kwa ugonjwa wa moyo. Makamu wa rais ambaye sasa ni rais Samia Suluhu alitangaza siku ya alhamisi juu ya kifo hicho kupitia televisheni ya taifa. Lakini huko nyuma tayari zilikuwa zimesambaa tetesi kuhusu aliko rais na kuhusu kuugua Covid-19. Mhariri huyu pia anasema Tanzania ni nchi pekee ya Afrika ambayo tangu Mei mwaka jana haijaweka wazi takwimu zake juu ya maambukizo ya virusi vya Corona,tangu pale rais Magufuli alipotangaza kwamba maombi yamevitokomeza virusi hivyo. Kadhalika alikuwa kiongozi pekee aliyeikataa katakata chanjo na badala yake akahimiza wananchi wajifukize kwa mitishamba na kupunguza hofu na akazipinga pia barakoa.

die tageszeitung nalo limeandika juu ya hali ya kutisha katika jimbo la Tigray la Kaskaziini mwa Ethiopia. Mauaji,uharibifu,uporaji yote yamefanywa na wanajeshi wa Ethiopia na wale wa Eritrea waliokwenda kwenye jimbo hilo.

Mhariri anasema mamilioni ya watu ya watu wa jimbo hilo wametenganishwa na Ulimwengu,na hakuna chombo huru kilichoruhusiwa kufika. Ethiopia iliweka wazi kwamba mgogoro katika jimbo lake hilo la kaskazini ni suala la ndani lakini hivi sasa ni suala linaloishughulisha kwa kiasi kikubwa jumuiya ya kimataifa. Marekani imebaini hivi karibuni kwamba kuna takasatakasa ya kikabila inayooendelea katika mapambano ya jimbo hilo na serikali ya Ethiopia inayosaidiana na wanajeshi wa nchi jirani ya Eritrea pamoja na makundi ya wapiganaji kutoka jimbo la Amhara wamebebeshwa dhamana. Hata mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrell amezungumzia juu uwezekano kwamba uhalifu wa kivita umetokea katika jimbo la Tigray.Na Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya ripoti za matukio ya ubakaji,mauaji makubwa na uharibifu mkubwa uliofanywa na pande zote.

Gazeti la Der Tagesspiegel limeandika juu ya hali ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja nchini Ghana na hasa katika mji mkuu Accra. Mhariri huyo anasema hali ya watu hao inazidi kuwa mbaya.Kile ambacho wachachama wa kundi la wanaojihusisha na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na mashirika ya haki za binadamu walichokihofia sasa kimeshaanza kuonekana. Ofisi zao zilivamiwa na baadhi ya wanachama wake wamekwenda mafichoni.Kiongozi wa kundi hilo la LGBT Alex Kofi Donkor na wanachama wengine walishambuliwa na kupewa vitisho vya kuuwawa: Na sio tu wanasakwa na polisi lakini wanatafutwa kwa udi na uvumba na wananchi.Mhariri anasema mwanzoni mwa mwaka huu kundi la wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na watetezi wao wamekuwa watu wanaopata vitisho vingi kwenye mitandao na nje ya mitandao.Hivi sasa sura zao zinawekwa wazi kwenye mitandao huku ikitolewa miito ya kutaka ofisi zao zifungwe na wakamatwe. Mkuu wao Donkor amekimbilia mji mwingine kwa usalama wake na kufungwa ofisi za kundi hilo kumeifanya Jumuiya ya kimataifa kuja juu. Katika barua ya wazi iliyosainiwa na watu maarufu 67 nchini Uingereza wenye asili ya Ghana akiwemo mwanamitindo mashuhuri Naomi Campbell ,Idriss Elba na Edward Enninnful wameeleza kutiwa wasiwasi na hatua ya kufungwa ofisi ya jamii hiyo ya wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.Wamemuomba rais Nana Akufo Ado na wanasiasa wengine wa Ghana kuilinda jamii hiyo ya mahoga na wasagaji.

Mwandishi: Saumu Mwasimba:

Mhariri: Daniel Gakuba