1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha kwanza kutokana na virusi vya corona Ufilipino

Sekione Kitojo
2 Februari 2020

Ufilipino imeripoti kifo cha mtu mmoja kutokana na virusi vya corona, cha kwanza kilichokwisha thibitishwa kutokana na ugonjwa huo nje ya  China.Takriban watu wawili walioondolewa na Ujerumani wameambukizwa virusi hivyo.

https://p.dw.com/p/3X9wJ
China | Coronavirus | Menschen mit Atemmaske in Peking
Picha: picture-alliance/AP Images/Y. Shimbun

Mchina  mmoja mwenye umri wa  miaka 44  alifariki nchini Ufilipino leo Jumapili (02.02.2020) kutokana  na matatizo yatokanayo  na virusi vya  corona, na  kwa mujibu wa  wizara ya  afya  ya  Ufilipino.

Philippinen Coronavirus Schutzmaskenverkauf
Watu wakinunua vibandiko vya usoni kuzuwia virusi vya corona nchini ChinaPicha: Getty Images/AFP/T. Aljibe

"Hiki ni kifo cha  kwanza  kuripotiwa  nje  ya  China," Muakilishi wa Shirika  la  afya  Ulimwenguni WHO, nchini  Ufilipino  Rabindra Abeyasinghe amewaambia  waandishi  habari  mjini  Manila.

Maafisa  wa  Ufilipino  wamesema  mtu huyo  alikuwa ni kutoka Wuhan, kitovu cha  virusi  hivyo nchini  China, na  aliwasili  nchini Ufilipino Januari 21.

Alilazwa hospitali  mjini  Manila na  kutengwa Januari 25 baada  ya kupata  homa, kukohoa  na  koo  kuuma. Baadaye  alipata kichomi kikali  na  kufariki baada  ya  kukaa  kwa  wiki  moja  hospitalini. Maafisa  wamesema  alikuwa  ameambukizwa  kabla  ya  kuwasili nchini  humo.

"Napenda  kusisitiza kuwa  hii ni  kesi muhimu ikiwa  haina  ushahidi wa  maambukizi  kutokea  ndani  ya  nchi," waziri  wa  afya Francisco Duque  amesema  katika  taarifa  kwa  vyombo  vya habari.

China Qingdao  Coronavirus  Desinfektion
Kazi ya kupulizia dawa dhidi ya virusi vya coronaPicha: picture-alliance/AP Photo/Chinatopix

Vifo vyaongezeka China

Mwanamke  Mchina  mwenye umri  wa  miaka  38 ambaye  alisafiri kwenda  Ufilipino pamoja  na  mtu  huyo  pia  ameambukizwa  na virusi  vya  corona na  amewekwa  katika  karantini  katika  hospitali hiyo.

Jana  Jumamosi (01.02.2020) maafisa  wa  afya  nchini  China wameripoti  vifo 45 kutokana  na  virusi  vya  corona, ambapo 32 kati  ya  vifo  hivyo  vimetokea  Wuhan, mji  mkuu  wa  jimbo  la Hubei. Vifo  hivyo  vipya  vilivyoripotiwa  vinafikisha  idadi jumla  ya vifo  kutokana  na  virusi  hivyo katika  China  bara  kutoka  watu 259 hadi 304.

Jumla  ya  watu  walioambukizwa  kwa  hivi  sasa  imefikia  watu zaidi ya  14,380, kwa  mujibu wa  maafisa  nchini  China.

Leo Jumapili (02.02.2020), benki kuu  ya  China  imesema  itaingiza kiasi  cha  euro  bilioni 156 katika  masoko wakati  masoko yatakapofunguliwa kesho Jumatatu kuimarisha  uchumi  wa  nchi hiyo kutokana  na  kuzuka  kwa  ugonjwa  huo nchini  humo.

Deutschland Frankfurt a.M. | Wuhan-Rückholung | Airbus A310 Kurt Schumacher | Bundeswehr
Ndege ya jeshi la Ujerumani ikiwasili mjini Frankfurt kutoka kuwachukua raia wa Ujerumani kutoka Wuhan ChinaPicha: Getty Images/AFP/T. Lohnes

Mji wa  pwani  wa  Wenzhou, kilomita  800 kutoka  Wuhan , umekuwa  mji  wa  kwanza  nchini  China  nje  ya  jimbo  la  Hubei kuchukua  hatua  za  vizuwizi. Mwanafamilia  mmoja  kutoka  kila kaya  anaruhusiwa  kwenda  nje  kila  baada  ya  siku  mbili kununua bidhaa za  mahitaji.

Zaidi  ya  nchi  kumi  na  mbili zimeripoti  kesi  za  virusi  vya  corona nje  ya  China. Hatua zinazoendelea  kuchukuliwa  ni  pamoja  na marufuku  ya  kusafiri  pamoja  na  watu  kuondolewa. Ujerumani , jana  Jumamosi  kupitia  ndege  ya  jeshi  la  Ujerumani imewarejesha  watu 124 kutoka  Wuhan hadi  Frankfurt, ikiwa  ni pamoja  na  raia  wa  Ujerumani 102.

Kumi  na  moja  walipelekwa  hospitali  mjini  Frankfurt, na kiasi wawili  wameambukizwa  na  virusi  hivyo.