1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha Fidel Castro: Dunia yatoa rambirambi

Daniel Gakuba
26 Novemba 2016

Kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Cuba Fidel Castro viongozi mbali mbali duniani waliomchukulia kama rafiki na mshirika wametoa salamu za rambirambi wakimsifu. Wacuba walioukimbia utawala wake, wamefurahia usiku kucha.

https://p.dw.com/p/2TIZL
Fidel Castro Besuch Schule 09.04.2013
Cuba imetangaza siku tisa za maombolezo kwa Fidel CastroPicha: REUTERS/Courtesy of Cubadebate

Kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Cuba Fidel Castro, viongozi mbali mbali duniani waliomchukulia kama rafiki na mshirika, wametoa salamu za rambirambi wakimsifu. Hata hivyo, wengine wengi, wakiwemo wacuba walioikimbia nchi yao wakati wa utawala wake, wamesherehekea kwa furaha usiku kucha, hususan mjini Miami, Marekani.

Katika salamu zake kwa rais wa Cuba Raul Castro, Rais wa Urusi Vladimir Putin  amesema, ''jina la kiongozi huyu wa kipekee, litakumbukwa kama nembo ya historia ya wakati wetu'', na kuongeza kuwa Fidel Castro alikuwa rafiki wa kutegemewa wa Urusi.

Kiongozi wa mwisho wa iliyokuwa Umoja wa Kisovieti Mikhail Gorbachev amesema ''Castro alikuwa nguzo ya Cuba iliyohimili vikwazo vikali kabisa vya Marekani, na kuiongoza nchi yake katika njia ya uhuru na maendeleo.

Kutoka China, rais wa nchi hiyo Xi Jinping amesema ''China imempoteza ndugu wa kweli''.

Msaada kwa wapigania uhuru

Libertadores Kuba Revolutionäre
Cuba ya Fidel Castro ilisaidia harakati za wanamapinduzi sehemu mbali mbali za duniaPicha: AP

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amemwagia sifa; ''Rais Castro alisimama upande wetu wakati wa vita vyetu dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi. Aliwahamasisha wacuba kujiunga nasi katika mapambano. Kama njia ya kumuenzi Castro, urafiki na uhusiano wa nchi zetu hauna budi kuendelezwa na kuimarishwa.

Uhusiano mzuri kati ya Cuba na Canada unaweza kusomeka katika salamu zilizotumwa na waziri mkuu wa Canada, Justin Trudeau, ambaye amesema, ''Nimepokea kwa huzuni kubwa habari za kifo cha Fidel Castro, rafiki wa muda mrefu wa Canada, na wa familia yangu.''

''Fidel Castro alijumuisha matumaini, na baadaye, kuvunjika moyo kutokana na mapinduzi ya Cuba'', amesema katika ujumbe wake Rais wa Ufaransa Francois Hollande. ''Kama mdau katika vita baridi, aliwakilisha fahari ya Cuba ya kukataa kuburuzwa'', amemalizia Hollande, bila shaka akimaanisha upinzani wa Cuba dhidi ya ubabe wa Marekani.

Waliokimbia Utawala wake washerehekea

USA Miami Reaktionen Tod Fidel Castro
Wacuba waishio Marekani wamesherehekea waliposikia habari za kifo cha CastroPicha: picture-alliance/dpa/G. De Cardenas

Lakini mjini Miami kusini Mashariki mwa Marekani, watu wa asili ya Cuba, ambao waliukimbia utawala wa Fidel Castro, wamejimwaga mitaani, wakisherehekea kwa furaha usiku kucha, wakiimba, ''Cuba huru, Cuba huru''.

''Inasikitisha kufurahia kifo cha mtu'', amesema Pablo Arencibia aliyeikimbia Cuba miaka 20 iliyopita, na kuongeza kuwa ''ingekuwa bora kama mtu huyo kamwe asingezaliwa''.

Kutoka Venezuela, nchi mshirika wa karibu kabisa wa Cuba katika Ukanda wa Ukanda wa Amerika Kusini na Karibeani, Rais Nicolas Maduro amesema, ''Ni jukumu letu kuendeleza ujumbe wa Castro, tukipeperusha bendera ya uhuru''.

Salamu nyingine za rambirambi zimetoka kwa Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy, ambaye amesema kupitia mtandao wa twitter, kuwa Fidel Castro atakumbukwa na katika historia kama kiongozi muhimu.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, amesema ''India inaomboleza kifo cha rafiki mkubwa''.

Ingawa Fidel Castro hakuwa na imani ya kidini, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema amesikitishwa na kifo chake, na kumuombea kupumzika kwa amani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri: Isaac Gamba