1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kibaki ataka mazungumzo na upinzani.

4 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CkF0

Nairobi.

Rais wa Kenya Mwai Kibaki ametoa wito wa utulivu na ametaka yafanyike mazungumzo na wapinzani wa kisiasa baada ya siku nyingine ya machafuko kutokana na mvutano wa matokeo ya uchaguzi. Rais Kibaki alilihutubia taifa katika televisheni wakati polisi na waandamanaji wakipambana katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.

Serikali imepiga marufuku mkutano uliotishwa na chama kikuu cha upinzani kikipinga matokeo hayo ya kuchaguliwa tena Kibaki.

Baada ya wafuasi wa kiongozi wa chama cha upinzani Raila Odinga kufyatuliwa mabomu ya kutoa machozi na maji kutoka kwa polisi, Odinga aliahirisha maandamano hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika leo Ijumaa. Wakati huo huo , mwanasheria mkuu wa serikali ya Kenya ametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru kuhusiana na matokeo ya uchaguzi.

Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani anayehusika na bara la Afrika Gendayi Fraser pia anatarajiwa kwenda nchini Kenya ili kuwahimiza viongozi wa nchi hiyo kutatua mzozo huo wa mkwamo wa kisiasa.

Mshindi wa nishani ya amani ya Nobel Askofu Desmond Tutu wa Afrika kusini nae yuko nchini Kenya kujaribu kupatanisha mzozo huo wa kisiasa uliozuka nchini Kenya.