1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM:Sudan yalaumiwa kuhusika na ghasia za Darfur

29 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBUp

Sudan inakanusha madai kuwa bado inahusika na ghasia katika eneo la Darfur baada ya kulaumiwa kukiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa mataifa katika eneo hilo linalozongwa na vita.

Wiki jana Shirika la Kutetea Haki za binadamu lililo na makao yake mjini London Amnesty International lilieleza kuwa Sudan bado inaendelea kukiuka vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa mataifa.Kulingana na shirika hilo ushahidi wa picha unaonyesha kuwa vifaa vya kijeshi vilipelekwa nchini Sudan mwezi Julai kupitia kiwanja cha ndege cha Al-Geneina kilichoko Darfur.

Wakati huohuo Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa Ban Ki Moon alieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la ghasia katika eneo la Darfur kulikoripotiwa visa vya kushambuliwa kwa vijiji.Kiongozi huyo anapanga kuzuru eneo la Darfur wiki ijayo.

Serikali ya Sudan kwa upande wake inasisitiza kuwa inataka amani kudumishwa katika eneo la Darfur na kutia juhudi zaidi ili kushawishi makundi yaliyojihami kujisalimisha.Kulingana na takwimu za Umoja wa mataifa zaidi ya watu laki mbili wamepoteza maisha yao na wengine milioni 2 kuachwa bila makao kwasbabu ya ghasia zilizodumu kwa muda wa miaka 4 kwenye eneo la Darfur.