1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM : Egaland azuiliwa kuingia kambi za wakimbizi

18 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCrh
Eneo la Golan
Eneo la GolanPicha: AP

Mkuu wa masuala ya misaada ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa Jan Egaland amekatisha ziara yake huko Dafur hapo jana na kurudi mjini Khartoum baada ya serikali kumzuwiya kuingia kwenye makambi ya wakaazi wa Dafur waliokimbia kubakwa,kuuwawa na kuteketezwa kwa nyumba zao.

Maafisa wa serikali ya Sudan wamesema usalama umeboreka huko Dafur tokea kufikiwa kwa makubaliano ya amani hapo mwezi wa Mei yaliosainiwa na makundi yote ya waasi isipokuwa moja tu.

Lakini maafisa wa usalama wa serikali wamemwambia Egaland ambaye alikuwako Dafur kwa ziara yake ya mwisho kwenye makambi ya wakimbizi kuwa ni hatari mno kwake kusafiri nje ya mji mkuu wa jimbo la Dafur.

Egaland akiusikitikia uamuzi huo wa serikali uliomzuwiya kwenda kwenye makambi hayo amesema anasikitika kwa sababu kazi yakea ni kuona vipi shughuli za msaada zinafanyika na vipi shughuli hizo zinazuiliwa jambo ambalo amesema hakuweza kulifanya.

Operesheni kubwa kabisa ya misaada duniani inafanyika huko Dafur ambapo wafanyakazi 14,000 wako kazini kuwasaidia zaidi ya watu milioni 3 wanaohitaji msaada.

Vitendo vya ujambazi wa barabarani,vikwazo vya urasimu kutoka serikalini na mapigano yanayoendelea vimekuwa vikikwamisha juhudi zao.