Kesi za washtukiwa wa majaribio ya shambulizi la kigaidi Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kesi za washtukiwa wa majaribio ya shambulizi la kigaidi Ujerumani

Ilikuwa kosa dogo tu katika utengenezaji wa mabomu ambalo limezuia mji wa Cologne hapa Ujerumani kukumbwa na mashambulizi mabaya ya mabomu sawa na yale ya London au Madrid.

default

Picha za kamera kwenye kituo cha treni mjini Cologne inayomwonyesha mtuhumiwa mmoja

Muda mfupi baada ya kuzuiliwa kwa mashambulizi haya kwenye treni za mikoa, mtuhumiwa wenye asili ya Lebanon alikamatwa ambaye kesi yake imeanza kusikilizwa leo mahakamani. Wakati huo huo, mahakama ya huko Lebanon ilimhukumu mtuhumiwa mwingine wa jaribio hilo kifungo cha miaka 12 na kuwaachia watuhumiwa wengine watatu.

Wiki tatu hivi baada ya kugunduliwa kwa masanduku haya mawili yenye mabomu katika treni za safari za mikoa hapo mwezi wa Julai mwaka uliopita, mtuhumiwa wa kwanza alikamatwa mjini Kile, Kaskazini mwa Ujerumani. Mlebanon huyu Yussef Mohammed al-Haj Dib aliyekuwa na umri wa miaka 22 wakati huo alipigwa picha za kamera kwenye kituo cha treni mjini Cologne akivaa shati ya timu la taifa la kandanda la Ujerumani lililokuwa na jina la “Ballack” na akibeba moja la masanduku haya.


Siku chache baada ya hapo, mtuhumiwa wa pili, Jihad Hamad mwenye umri wa miaka 20 alijisalimisha nchini Lebanon. Yeye pia alipigwa picha akiliweka sanduku katika treni hiyo. Kesi ya Jihad Hamad ilianza mwezi wa Aprili mwaka huu nchini Lebanon na Jihad alikubali kosa lake, chanzo alisema alitaka kulipiza kisasi kutokana na pich za katuni za kumkashifu mtume Mohamed zilizochapishwa katika magazeti kadhaa ya Ulaya na ambazo zilichukuliwa kama matusi dhidi ya madhehebu ya Kiislamu. Leo hii, mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka 12 na kazi ngumu. Kulingana na wakili wake, watuhumiwa wengine watatu waliachiliwa huru.

Leo hii pia, kesi dhidi ya mtuhumiwa mwingine Yussuf Mohamed ilianza kusikilizwa leo mjini Düsseldorf, Ujerumani. Mwendeshaji mashtaka wa serikali Horst Salzmann alisema: “Baada ya matamshi ya mshtakiwa mwenzake Jihad Hamad huko Lebanon tunaamini kwamba washtakiwa walikuwa na nia ya kuwaua watu wengi iwezekanavyo.”


Bw. Salzmann alisema pia mpango wa washtakiwa ulikuwa kuzishambulia treni mbili wakati mmoja na halafu kukimbia nje ya nchi.


Wakili wa mshtakiwa, Bw. Johannes Pausch, naye alisema kwa upande wake atajaribu kuthibitisha kwamba kasoro iliyokuweko katika ujenzi wa mabomu haya iliyozuia mabomu kuripuka ilifanywa kwa makusudi. Alisema: “Walikamilisha tu asilimia 90 ya kazi ya utengenezaji, asilimia 10 hazikukamilishwa. Hilo ni kasoro lililowazi kabisa na tutajaribu kutoa ushahidi kwamba kosa hilo lilifanywa kwa makusudi, kwa hivyo waliachana na mpango wao wa mashambulizi.”


Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea hadi mwaka ujao.

 • Tarehe 18.12.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CdJn
 • Tarehe 18.12.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CdJn
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com