1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Taylor yaahirishwa.

Mohamed Dahman25 Juni 2007

Kesi ya uhalifu wa vita ya Charles Taylor leo imeahirishwa kwa wiki moja baada ya rais huyo wa zamani wa Liberia kususia mahkama kwa mara nyengine tena kutokana na matatizo na mawakili wake wa utetezi.

https://p.dw.com/p/CHCG
Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor aisusia tena mahkama ya mjini The Hague.
Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor aisusia tena mahkama ya mjini The Hague.Picha: AP

Akiahirisha kesi hiyo hadi tarehe 3 mwezi wa Julai hakimu anayesimamia kesi hiyo katika mahkama ya kimataifa ya mjini The Hague Uholanzi Julia Sebutinde amesema kesi hiyo itaanza kwa kusikiliza mashahidi wa upande wa mashtaka.

Mahkama hiyo pia imeamuru kwamba Taylor apatiwe timu ya ushauri ya mawakili wa utetezi ya muda wakati juhudi zikifanyika kumpatia timu inayofaa ya mawakili wa utetezi.

Taylor mwenye umri wa miaka 59 anakabiliwa na mashtaka 11 ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu uliotendeka wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1991 hadi mwaka 2001 nchini Sierra Leone.

Akiwa kiongozi wa kwanza wa nchi barani Afrika kushtakiwa kwa uhalifu wa vita Taylor alisusia ufunguzi wa kesi hiyo wiki tatu zilizopita mbele ya Mahkama hiyo Maalaum kwa ajili ya Sierra Leone inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na amemtimuwa wakili wake kwa hoja kwamba alikuwa hana nafasi ya kupatiwa haki kwenye kesi hiyo.

Rais huyo wa zamani leo tena hakuwepo mahkamani na kumfanya hakimu Sebutinde atowe karipio kwa kusema kwamba mshtakiwa hana chaguo la kwenda mahkamani anapotaka na kwamba anawajibika kufika mahkamani wakati wote.

Mojawapo ya malalamiko makuu ya Taylor ni kwamba hakupatiwa fedha za kutosha kuweza kuwa na timu nzuri ya mawakili.Hakimu alikubaliana na dai hilo na ameamuru mrajisi wa mahkama hiyo kutafuta fedha zaidi.Kabla ya kuanza kwa kesi hiyo mahkama imegunduwa kwamba Taylor alikuwa fukara na kwamba alikuwa hawezi kuwalipia mawakili wake.

Hakimu Sebutinde amekaririwa akisema kwamba iwapo mahkama hiyo inatarajiwa kuendesha kesi itakayozingatia haki inabidi itowe fedha za kutosha na mawakili wa utetezi.

Mwendesha mashtaka mkuu wa Sierra Leone Stephen Rapp amesema hana tatizo na kuahirishwa kwa kesi hiyo na kwamba wameridhika kuwa Taylor hatonufaika na tabia yake hiyo ya kukwamisha shughuli za mahkama hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Human Right Watch uamuzi huo wa mahkama unaonyesha matatizo ya bajeti kwa mahkama hiyo kwa ajili ya Sierra Leone.

Mahkama hiyo inagharimiwa kwa michango ya hiari kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Takriban watu 200,000 wameuwawa katika mzozo wa Sierra Leone ambapo waasi walikuwa wakiwakata mikono,masikio na pua maelfu ya watu.

Taylor inadaiwa kuwa alikuwa akiwapatia silaha,kuwafunza na kuwadhibiti waasi hao wa kundi la RUF lililohusika na unyama huo kwa kiasi kikubwa na badala yake kiongozi huyo kupatiwa almasi ambayo kima chake hakijulikani kwa ajili ya kugharamia vita.

Taylor ambaye alikuwa rais wa Liberia kunzia mwezi wa Augusti mwaka 1997 hadi Augusti mwaka 2003 amekanusha madai yote hayo.

Alikamatwa hapo mwezi wa Machi mwaka 2006 na kupelekwa Uholanzi kutoka Sierra Leone kutokana na wasi wasi wa kuzuka kwa mapigano mapya ingelikuwa kesi hiyo imesikilizwa mjini Freetown.