1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Mubarak ni historia kwa Misri

4 Agosti 2011

Kesi dhidi ya kiongozi wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak, ni aibu kwake na chama chake. Waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Habib al Adly, pamoja na maafisa wengine sita wa serikali ya Mubarak wamepandishwa kizimbani

https://p.dw.com/p/12BBI
Rais wa zamani wa Misri, Hosni MubarakPicha: Egyptian State TV/AP/dapd

Kuliandikiwa historia jana nchini Misri. Kwa mara kwanza katika historia ya taifa hilo kiongozi aliyeondolewa madarakani alilazimika kukabiliana na aibu ya kufikishwa katika mahakama ya nchi yake hadharani, tena mbele ya wananchi wake! Hosni Mubarak ambaye kwa miaka 30 aliingoza Misri kama kiongozi aliyekuwa akipitisha maamuzi kuhusu mustakabali wa nchi hiyo, alisimama kizimbani, au kwa maneno sahihi, alilala kizimbani. Rais huyo wa zamani alifikishwa mahakamani akiwa kwenye machela pamoja na wanawe wawili wa kiume na waziri wake wa zamani wa mambo ya ndani, Habid al Adly, na maafisa wengine wa serikali yake.

Picha za aina hiyo nchini Misri sio jambo geni kwani zimekuwa zikionekana wakati magaidi au wapinzani wa serikali wanapofikishwa mahakamani. Zimeshaonekana pia picha za wafuasi wa chama cha Udugu wa kiislamu na wafuasi wa upinzani unaopigania demokrasia nchini Misri. Kwa miaka mingi walifuatiliwa na kukamindamizwa na maafisa wa usalama wa utawala wa Mubarak.

Lakini sasa mambo yamemgeukia mwenyewe Mubarak! Amelazimika kusimama mbele ya majaji na umma. Hata hivyo, kesi hii haihusiani na hatua ya kulipiza kisasi, bali haki kwa wahanga wa maandamano ya mapinduzi ambao waliuwawa au kujeruhiwa kufuatia amri ya rais Mubarak. Inahusu haki kwa Wamisri ambao kwa miongo mingi wamekuwa wakizuiliwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa nchini mwao.

Aibu kutokana na kesi hii iliyofanyika hadharani inawapata moja kwa moja Mubarak na wanawe pamoja na wafuasi wa chama chake. Wengine wengi wenye hatia na walionufaika kutokanana utawala wa Mubarak wanasubiri kufikishwa pia mahakamani. Kwa sasa ni bayana kwamba wengi wao, ambao wanabeba dhamana kwa makosa yaliyotokea, hawatafikishwa mahakamani. Kwa mfano, wanajeshi ambao kwa miongo kadhaa waliweza kumuunga mkono na kumlinda Mubarak na kunufaika kutokana na utawala wake. Sasa wako katika madaraka na hakuna ajuaye ikiwa kweli watakabidhi madaraka kwa serikali itakayochaguliwa kwa njia ya demokrasia.

Kufuatia siku ya kihistoria ya jana nchini Misri viongozi wa nchi na serikali za mataifa ya magharibi wanapaswa kutafakari ikiwa haikuwa pia siku ya aibu kwao.

Mwandishi: Marx, Bettina (DW Berlin)

Mhariri: Othman Miraji