1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Khodorkovsky haikuwa ya haki

28 Desemba 2010

Mada kuu katika magazeti ya Ujerumani hii leo inahusika na hukumu iliyotolewa dhidi ya tajiri mkubwa wa zamani nchini Urusi, Mikhail Khodorkovsky.

https://p.dw.com/p/Qkd7

Basi tukianza na hukumu iliyotolewa kwa Khodorkovsky, gazeti la AUGSBURGER ALLGEMEINE linalosema:

Kesi ya Mikhail Khodorkovsky wala haikuwa ya haki- ushahidi ni matamshi ya Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin kuwa mshtakiwa huyo akutikane na hatia. Na mwito wa Rais Dmitry Medvedev kupinga kuishinikiza mahakama si kingine isipokuwa kutoa sura kuwa mahakama ina uwezo wa kujiamulia yenyewe.Lakini ukweli ni tofauti kabisa. Hata malalamiko ya serikali za magharibi hayataoweza kubadili cho chote. Kwani Putin anafahamu vizuri kuwa Urusi ni muhimu kama soko na muuzaji wa nishati.

Kwa maoni ya gazeti la MANNHEIMER MORGEN,Urusi iliyo muuzaji mkubwa wa nishati si nchi kuu pekee ambayo kwa sababu za kisiasa hakuna anaetaka kuikwaruza.

Kwani kidemokrasia,China ikilinganishwa na Urusi,ipo katika enzi ya kale lakini kiuchumi inazidi kuwa na usemi duniani.Kwa hivyo si Umoja wa Ulaya wala Ujerumani zinazotaka kuhatarisha uhusiano wake na mataifa hayo makuu mawili.

Lakini hiyo isimaanishe kuwa nchi hizo ziachiliwe kufanya zipendavyo kwa sababu ya umuhimu wake wa kiuchumi.Mara kwa mara Urusi na China zinakiuka haki za binadamu.

Kwa hivyo, Khodorkovsky au raia wa China, Liu Xiabao alieshinda zawadi ya amani ya Nobel, ni wahanga maarufu tu wakati wengine wasiojulikana wakiendelea kuteketea katika jela.

Sasa hebu tutupie jicho mada nyingine iliyoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii.Mageuzi katika mfumo wa afya,hasa kuhusu wagonjwa wenye bima ya afya ya serikali.Gazeti la HESSISCHE-NIEDERSÄCHSICHE ALLGEMEINE limeandika hivi:

Inavutia ikiwa hospitali,wagonjwa wote wenye bima ya afya ya serikali watalazwa katika chumba chenye vitanda viwili tu.Hiyo lakini ni kawaida katika hospitali mpya. Hata hivyo, hapa inafaa kuuliza iwapo lengo hilo litaweza kweli kutekelezwa.

Kwani hospitali zimelazimishwa na serikali kupunguza matumizi yake. Sasa watawezaje kutimiza lengo hilo bila ya kupata gharama zaidi? Je, viwango vya juu vya tiba ndio viwe muhanga?

Hakuna atakaetaka hilo. Kwa hivyo, ionekanavyo, hali itabakia kama ilivyo, yaani anaetaka kuwa katika chumba chenye watu wachache atapaswa kujilipia mwenyewe.

Mwandishi:P.Martin/DPA

Imeptiwa:Josephat Charo