1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawakili wa wahanga walalamika

22 Julai 2015

Kesi ya rais wa zamani wa Chad Hissène Habré mbele ya mahakama maalumu ya Afrika mjini Dakar Senegal, imeakhirishwa hadi septemba 7.Kiongozi huyo wa zamani wa kiimla anapinga kujitetea akihoji haitambui mahakama hiyo.

https://p.dw.com/p/1G2W6
Muimla Hissene Habre akifuatwa na wanajeshi baada ya kusikilizwa na jaji mmoja mjini Dakar-SenegalPicha: AFP/Getty Images

Kutokana na azma ya Hissène Habré ya kuisusia kesi hiyo inayoangaliwa kama mfano wa kuigizwa katika mapambano dhidi hali ya ukosefu wa haki na sheria barani Afrika, korti hiyo maalum imeamua kumpatia mtuhumiwa mawakili watatu wa kutoka Senegal waliopatiwa muda wa siku 45 kudurusu na kuijua kikamilifu kadhia hiyo.

Mawakili hao wameteuliwa na mahakama kutokana na orodha iliyopendekezwa na mwenyekiti wa baraza la mahakimu wa korti hiyo maalum-amesema mmoja wa mawakili hao,Mbaye Sène aliyehakikisha watatekeleza jukumu lao kuambatana na sheria.

"Tunaanza kazi yetu tangu sasa ili kuhakikisha tutaitetea ipasavyo kadhia hii.Hatutokwenda mahakamani kama mashahidi tu" amesisitiza wakili Sène.

Mawakili wa upande wa wahanga wameitahadharisha mahakama hiyo maalum dhidi ya hatari inayotokana na kipindi hicho cha siku 45.Wanahisi mtuhumiwa anaweza kukitumia "kuivuruga kesi"-kwa kuwakataa mawakili walioteuliwa,mara tu baada ya kesi kuanza upya kusikilizwa.

Kuakhirishwa kwa kesi hiyo kunaweza kumfungulia njia ya kuvuruga,kukorofisha na hata kufuja chombo cha sheria ambacho hataki kukitambua,kwasababu anahofia hukmu itakuwa ya aina gani-amesema wakili William Bourdon,mfaransa anaewatetea wahanga wa utawala wa Hissène Habré.

Zaidi ya watu 40.000 wameuwawa katika utawala wa habré

Akishikiliwa kizuwizini nchini Senegal tangu miaka miwili iliyopita,Hissène habré anatuhumiwa kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinaadam,uhalifu wa vita na uhalifu wa mateso.Akikutikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 30 jela na kazi za lazima milele.

Tschad Präsident Idriss Deby 3.4.2014
Rais wa sasa wa Chad,Idriss DebyPicha: Thierry Charlier/AFP/Getty Images

Utawala wake wa mabavu umeangamiza maisha ya watu 40 elfu-kwa mujibu wa tume ya uchunguzi ya Tchad-zaidi ya wahanga 4000 wamejiunga na upande wa mashtaka dhidi yake.

Mwenyekiti wa jumuia ya wahanga dhidi ya mateso na ukandamizaji wa kisiasa nchini Tchad,Clément Abaifouta ameelezea masikitiko yake kumuona Hissène Habré akikataa kusema chochote mahakamani."Inasikitisha kuona jinsi anavyodharau na kutemea mate kumbu kumbu za wahanga." amesema Abaifouta.

Reed Brody wa shirika la Human Rights Watch anahisi muhimu ni kuona kesi inafanyika na kuhakikisha Habré anapatiwa mawakili wazuri.

Kesi ya haki haiwezi kufanyika bila ya mawakili wa mshitakiwa

Mwenyekiti wa korti hiyo maalum ya Afrika, Gberdao Gustav Kam,wa Burkina Faso ameshawaambia mawakili walioteuliwa ni jukumu lao kutetea masilahi ya Hissène Habré hata kama mwenyewe hataki,na kwamba ni jukumu la korti kuhakikisha kesi inafanyika kwa njia ya haki na bila ya mapendeleo."

Senegal Prozess gegen Hissene Habre in Dakar Pressekonferenz
Wahanga wa utawala wa kimabavu wa Hissène Habré katika ukumbi wa korti mjini Dakar-SenegalPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Blackwell

Kwa maoni ya mtaalam wa sheria za kimataifa za makosa ya jinai,Hugo Moudiki Jombwe,kuteuliwa mawakili wa kumtetea Habre ni tukio la lazima."Kesi haiwezi kuendelea bila ya mawakili wa mshitakiwa na hata kama uamuzi wa kuakhirisha kesi hiyo umewakera baadhi ya wahanga-uamuzi huo umepitishwa ili kuheshimu kanuni za kesi huru na ya haki.Na hilo pia ni kwa masilahi ya wahanga."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:Josephat Charo