1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta azindua rasmi ripoti ya BBI

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi.28 Novemba 2019

Rais Uhuru Kenyatta amezindua rasmi ripoti ya jopo la Maridhiano inayotarajiwa kupigiwa kura ya maoni na hatimaye kuidhinishwa na bunge.

https://p.dw.com/p/3To0p
Kenia Building Bridges Initiative (BBI)
Picha: AFP/T. Karumba

Cheche za siasa zilizimwa na joto lake likashuka nchini kwenye hafla iliyowaleta mahasimu na marafiki wa kisiasa pamoja katika ukumbi wa Bomas. Aidha wawakilishi 100 kutoka kwenye kauti 47 walihudhuria uzinduzi wa ripoti ya BBI ambayo huenda ikapigiwa kura ya maoni na Wakenya.

Kwenye mfumo wa utawala, ripoti hiyo inapendekeza Rais kumchagua Waziri Mkuu kutoka kwa chama chenye viti vingi bungeni ama muungano mkubwa bungeni ambaye atachukua nafasi hiyo baada ya kuidhinishwa na bunge.

Hata hivyo nafasi ya Waziri Mkuu wakati huu haina mamlaka mengi, kwani rais anaweza akamfuta kazi wakati wowote. Aidha anaweza akapigwa kalamu kupitia kura ya kutokuwa na imani naye kwenye bunge. Jopo la Maridhiano lilibuni nafasi hiyo kwa lengo la kumtuza mshindani wa pili kwenye uchaguzi wa urais na kuzuia ghasia za baada ya uchaguzi.

Hata hivyo suala la Tume Huru Ya Kusimamia Uchaguzi na Mipaka kuendesha uchaguzi huru haujaangaziwa kwani mara nyingi limekuwa chimbuko la ghasia hivyo huenda uchaguzi mkuu ujao ukakumbwa na utata, kwani kabla ya salamu za heri upinzani ulitaka marekebisho kwenye mchakato wa kusimamia uchaguzi.

Kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya maridhiano BBI katika ukumbi wa Bomas Nairobi Kenya
Kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya maridhiano BBI katika ukumbi wa Bomas Nairobi KenyaPicha: AFP/T. Karumba

Kwa sasa upinzani unayumbayumba haijulikani iwapo upo ama haupo ripoti ya BBI inaupa upinzani mashiko na kuiwajibisha serikali. Mapendekezo yakiidhinishwa upinzani utakuwa na kiongozi wake bungeni kinyume na ilivyo sasa.

Wakenya bado wana hofu kuhusiana na utekezaji wake.

Ripoti hiyo inapendekeza kuwa rais asalie kuwa kiongozi wa serikali, naibu rais awe msaidizi wake ambaye atakuwa mgombea mwenza kwenye uchaguzi mkuu. Wengi walidhani kuwa nafasi nyingi za uongozi ambazo zimechangia matumizi makubwa ya fedha serikalini zitapunguzwa. Hata hivyo hilo halijafanyika, wakenya wataendelea kugharamia mishahara minono na marupurupu ya zaidi ya waakilishi 400. Yusuf Haji, mwenyekiti wa Jopo la Maridhiano amesema ingawa Wakenya wengi walionyesha kufurahishwa na hatua hiyo, lakini walihoji iwapo yote yaliyomo yatafanyiwa kazi.

Baadhi ya viongozi wa kisiasa na wageni waliohudhuria uzinduzi wa ripoti hiyo ya maridhiano (BBI) wakiwa katika ukumbi wa Bomas mjini Nairobi Kenya
Baadhi ya viongozi wa kisiasa na wageni waliohudhuria uzinduzi wa ripoti hiyo ya maridhiano (BBI) wakiwa katika ukumbi wa Bomas mjini Nairobi KenyaPicha: AFP/T. Karumba

Aidha ripoti hiyo imependekeza kuongezwa kwa mgao wa fedha katika kaunti kwa asilimia 35 ya mapato ya taifa. Kwa sasa kaunti hupokea asilimia 15 tu ya mapato hayo.

BBI pia inapendekeza kupiga marufuku maafisa wa serikali kufanya biashara na serikali kama njia ya kukabiliana na ufisadi. Aidha wafichuzi wa kashfa za ufisadi watakuwa wakipokea asilimia tano ya fedha hizo. Wakenya wameelezea hisia zao baada ya uzinduzi rasmi, wakisema wana imani kwamba itasaidia kupambana na ufisadi, ingawa wengine walisita kuweka imani yao.

Ili kukabiliana na migomo ya mara kwa mara katika sekta ya afya, ripoti hiyo inapendekeza kubuniwa kwa Tume Huru ya Afya ambayo itasimamia sekta hiyo kwenye kaunti. Hata hivyo kama tu ripoti za tume nyingine suala la utekelezaji linasilia kuwa changamoto kwa taifa ambalo linasemekakana kuwa na moja ya katiba bora ulimwenguni ambayo imenajisiwa na viongozi. Safari ya BBI imefikia kituo huku safari nyingine ya kusoma na kufanya maamuzi kwa wakenya ikianza.