1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta arefusha muda wa vizuizi kwa siku 60

Shisia Wassilwa29 Septemba 2020

Rais Uhuru Kenyatta ametangaza kurefusha kwa siku nyingine 60 vizuizi vya kukabiliana na janga la virusi vya corona nchini Kenya, na kuongeza kuwa shule bado hazitafunguliwa hadi usalama wa wanafunzi uzingatiwe.

https://p.dw.com/p/3j9Vn
Kenia Uhuru Kenyatta
Picha: imago/i Images

Kwenye kongamano lililowaleta pamoja wadau mbali mbali kutathmini janga la virusi vya corona, rais Kenyatta alisema kuwa masharti ya kutotoka majumbani sasa yataanza kutekelezwa saa tano usiku hadi saa kumi alfajiri.

Awali masharti hayo yalikuwa yakitekelezwa kuanzia saa tatu usiku. Aidha mabaa na vilabu yameruhusiwa kufungua tena, baada ya kufungwa kwa miezi sita huku yakizangatia masharti yaliyotangazwa na wizara ya afya.

Soma pia: Kenyatta aongeza tena vizuizi dhidi ya corona

Kuhusu suala la tarehe ya kufunguliwa kwa shule, rais Kenyatta hakutaja tarehe makhsusi, akisema kuwa ni bora kwa usalama wa wanafunzi kuzingatiwa kabla ya kufunguliwa kwa shule.

Kenia Isolationsbetten im Coast general hospital
Kenya imerikodi visa 38,168 vya maambukizi ya covid-19, huku watu 700 wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.Picha: DW/F. Musa

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha atatangaza tarehe hiyo, pindi, usalama katika shule zote utakapozingatiwa. Jumatatu walimu wa shule, walianza kufanya maandalizi ya kufunguliwa kwa shule zao.

Katika baadhi ya mataifa jirani, shule zilishafunguliwa. Mataifa hayo ni pamoja na Tanzania na Sudan Kusini. Hadi kufikia sasa kenya imerekodi visa 38,168 vya virusi vya Corona. Kati ya visa hivyo, wagonjwa 24691 wamepona huku vifo vikiwa 700.

Soma pia: Corona yazua hofu katika bunge la Kenya

"Lazima tutambue na tukubaliane, kwamba licha ya changamoto kubwa zilizotukumba, janga ambalo limetokea halijakuwa na athari kubwa tuliyoitarajia. Kwa hilo tunamshukuru Mungu,” alisema waziri wa afya wa Kenya Mutahi Kagwe.

Uhalifu wapungua pakubwa

Aidha, idadi ya waumini makanisani na wanaoruhusiwa kushiriki kwenye shughuli za mazishi pia imeongezwa, kutoka 100 hadi 200. Hayo ni kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na Baraza la Dini zenye Imani tofauti.

Kenia Gesundheitsminister Mutahi Kagwe
Waziri wa afya wa Kenya Kagwe Mutahi.Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Hata hivyo masharti yaliyotolewa na wizara ya Afya ya kuvalia barakoa, kunawa mikono na kukaa umbali wa mita moja u nusu yatazingatiwa. 

Soma pia:Kenya yapiga marufuku usafiri katika miji iliyoathirika na virusi vya corona 

Kwa kipindi cha miezi sita, tangu masharti hayo, yaanze kutekelezwa visa vya uhalifu vimepungua kwa asilimia 21, huku misongamano ya magari ikipungua pia kwa wastan wa asilimia 10.

Suala jingine ambalo lilijadiliwa kwenye kongamano hilo ni iwapo mikakati ya kukabiliana na janga la Corona ilifanikiwa, licha ya visa hivyo kuongezeka.

Soma pia: Jumla ya wauguzi 16 Kenya wapoteza maisha kutokana na COVID-19

Aidha suala la mikakati hiyo kutumika tena siku zijazo ilijadiliwa. Kwa mara nyingine tena makamu wa rais William Ruto, alikosa kuhudhuria kongamano hilo ambalo, lilikuwa la taifa.